Home news BAADA YA KUPANGWA NA TIMU YA KINA CHAMA CAF…SIMBA WAJA NA MKAKATI...

BAADA YA KUPANGWA NA TIMU YA KINA CHAMA CAF…SIMBA WAJA NA MKAKATI HUU WA KIMFYA…WAIOTA ROBO KWANZA…

 


MABOSI wa Simba wamelichungulia Kundi D iliyopangwa timu yao katika mechi za michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika sambamba na ratiba ya mechi zao na fasta wakaifanyia tathmini haraka na kupata matumaini kuwa watapenya hadi robo fainali.

Sio hatua hiyo tu, kwa jinsi walivyopania msimu huu kimataifa wanaamini watafika mbali zaidi. Kundi hilo mbali na Simba, lina timu nyingine tatu – RS Berkane ya Morocco, Asec Mimosas (Ivory Coast) na US Gendarmerie Nationale (Niger).

Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, Mulamu Nghambi amesema  kwa namna kundi lao lilivyo na uzoefu walionao hawana presha yoyote na imani yao ni kufika mbali baada ya malengo katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kutotimia.

“Berkane na Asec ni timu ambazo tunazifahamu vyema, ingawa kidogo hawa Gendarmerie hatuna taarifa zao za kutosha, ila kwa ukubwa na uzoefu wa Simba sidhani kama hilo ni tatizo sana naamini tuna nafasi kubwa ya kuingia hatua ya robo fainali,” alisema.

“Asec walikuwa tishio zamani lakini kwa sasa wachezaji wengi wazuri wa Afrika Magharibi wanakimbilia Ulaya, hivyo klabu zao hazina wachezaji bora kiasi hicho kulinganisha na kikosi cha Simba na Berkane sio tishio sana na tunaweza kupata matokeo mazuri dhidi yao.”

Nghambi alisema changamoto iliyopo mbele yao ni suala la usafiri na taratibu za kuingia katika nchi ambazo timu zilizopo kundi hilo zinatoka, lakini ana uhakika haiwezi kuwa shida kwao.

“Hizo nchi zote usafiri wa kwenda huko ni wa ndege za kuunganisha ambapo safari ya kwenda inaweza kuwa hata ya siku mbili au tatu. Hivyo kuna uwezekano mkubwa tukalazimika kutumia usafiri wa ndege ya kukodi kwani kuna muda mfupi kutoka nchi moja hadi nyingine.

“Ivory Coast tutakapoenda kucheza na Asec kwa mfano tumeshawahi kwenda. Ni nchi ambayo ina changamoto kubwa katika masuala ya utaratibu na hata Niger naamini iko hivyo, lakini kama ambavyo nimesema awali kuwa Simba ni timu kubwa na inafahamu hilo na haliwezi kutusumbua,” alisema Nghambi.

SOMA NA HII  SHINDA KIWEPESI ZAIDI NA SLOT YA 777 KUPITIA CASINO YA MERIDIANBET

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa baada ya droo ya juzi, Simba itaanzia nyumbani ikiivaa Asec Mimosas, Februari 13 mwakani na siku chache baadaye itaifuata Gendarmerie, mchezo utakaochezwa kati ya Februari 18-19. Februari 25 au 26 Simba itacheza tena ugenini dhidi ya RS Berkane watakaorudiana nao jijini Dar es Salaam kati ya Machi 11 na12 kisha itakwenda Abidjan kurudiana na Asec Mimosas kati ya Machi 18 na 19. Wekundu hao watakamilisha ratiba kati ya Aprili 1 na 2 nyumbani kucheza na US Gendarmerie.

Nghambi alisema wamepanga kuhakikisha Simba inapata ushindi katika mechi mbili za mwanzo, kwani ndizo zitawaweka katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya robo fainali.

“Siku zote mechi mbili za kwanza za makundi ndizo zinaamua kama unaenda robo fainali au hauendi. Hata msimu uliopita, mechi mbili za mwanzo ndizo zilichangia kutufanya tuongoze kundi.

“Kwa maana hiyo tukishinda nyumbani dhidi ya Asec na kisha ugenini dhidi ya Gendarmerie tutakuwa katika nafasi nzuri ukizingatia mechi mbili zitakazofuata zitakuwa dhidi ya Berkane nyumbani na ugenini,” alisema Nghambi. Ni mara ya kwanza kwa Simba kukutana na RS Berkane na Gendarmerie, lakini imekutana na Asec Mimosas katika makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2003 ambapo Simba ilishinda bao 1-0 nyumbani na ugenini ikapoteza 4-3.