Home news KISA KUKABWA MPAKA KIVULI NA MABEKI WA SIMBA…MAYELE ASHINDWA KUJIZUIA..AMTUPIA LAWAMA...

KISA KUKABWA MPAKA KIVULI NA MABEKI WA SIMBA…MAYELE ASHINDWA KUJIZUIA..AMTUPIA LAWAMA ‘FEI TOTO’…


MJADALA mkubwa wa mechi ya Simba na Yanga iliyomalizika kwa suluhu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumamosi iliyopita umeendelea kuwa ni ile bato ya straika Fiston Mayele na mabeki Joash Onyango na Henock Inonga na sasa straika huyo kazungumza kitu.

Mashabiki wengi wanazungumzia kuhusu Inonga na Onyango kumfunika Mayele, lakini straika huyo Mkongomani amesema sababu ni kwamba alisimama mbele peke yake, tofauti na mechi nyingine alizokuwa anacheza pacha na Feisal Salum ‘Fei Toto’, ambapo mmoja akikabwa mwingine anapata nafasi ya kufunga.

Alisema katika dabi hiyo, alikuwa mbali na Fei Toto, jambo lililowapa upenyo mabeki hao, kumkaba kila alipokuwa anakwenda na mpira mbele.

“Nimezoea kucheza mbele na Fei Toto, ila kwenye dabi alikuwa mbali, ndio maana Onyango na Inonga ilikuwa rahisi kukutana na mimi mbele nikiwa kwenye harakati za kwenda kufunga ama walikuwa wananiona kirahisi,” alisema Mayele na akaongeza kuwa;

“Mbali na kukabwa na hao mabeki, Simba ilicheza kwa ushindani mkali kwasababu ni mechi inayoleta huzuni na furaha Tanzania, hivyo kila mchezaji alikuwa anapambania furaha ya mashabiki wake kwa kadri tulivyoweza,” alisema.

Sababu nyingine aliyotaja ya kukabwa na mabeki hao ni kutokana na kuwafunga mechi ya Ngao ya Jamii, kitu ambacho kilikuwa hakikwepeki kwa mabeki gao kumkamia.

“Kama unavyojua dabi inavyokuwa ngumu na utani wa mashabiki, mabeki walitambua wazi nikiwafunga wangekuwa wateja wangu, ingawa nilipambana kwa kadri nilivyoweza, unaona kuna wakati niliteleza wakati nakwenda kufunga, lakini yote ni matokeo ya mpira, tuache kazi nyingine ziendelee,” alisema.

Alisema uwezo wake wa kufunga mabao na kuwasumbua mabeki ndio uliowafanya Onyango na Inonga kuonekana kufurahia sana yeye kutorudia sherehe yake ya kufunga kama alivyowatungua 1-0 kwenye Ngao ya Jamii.

STAILI YA KUSHANGILIA

Mayele mwenye mabao matatu hadi sasa, alisema kitendo cha mashabiki kupokea staili yake, kinampa faraja na kujiona kama yupo nchini kwao DR Congo.

“Nilitamani sana niifunge Simba ili mashabiki wangu waendelee kufurahia staili ya ushangiliaji wangu, maana naiona inavyotamba maeneo mbalimbali hapa Tanzania, ikiwemo makanisani,” alisema Mayele na akaongeza kuwa;

SOMA NA HII  MASAU BWIRE AFUNGUKA NAMNA ALIVYOPEWA OFA SIMBA, AMTAJA MANARA

“Dabi imepita, napaswa kuwekeza nguvu kwenye majukumu yaliyopo mbele ambayo yataifanya Yanga ifikie malengo yake na mashabiki wetu kucheka huko mtaani, kikubwa mashabiki wetu waendelee kutuunga mkono kwa sababu kuna mazuri yanakuja mbele.”