Home news KUHUSU ISHU YA WAWA KUTEMWA AU AACHWE…PAWASA AIBUKA NA HILI..ATOA ONYO KALI…

KUHUSU ISHU YA WAWA KUTEMWA AU AACHWE…PAWASA AIBUKA NA HILI..ATOA ONYO KALI…


KIKOSI cha Simba jana kilitua salama jijini Mwanza na fasta kutimkia Bukoba kwa ajili ya mechi yao ya Ligi Kuu dhidi ya Kagera Sugar ambao ulighairishwa kutokana na wachezaji wa timu zote mbili kukumbwa na ugonjwa wa mafua, lakini kukiwa na tetesi la kupitishwa panga kwa baadhi ya nyota wake, huku jina la Pascal Wawa likitajwa na sasa baadhi ya wadau wameibuka wakiionya Simba.

Wadau hao wameionya Simba kuwa wasithubutu kumtema beki huyo, licha ya kwamba anaonekana kapoteza namba kikosi cha kwanza, lakini wadau mbalimbali wa soka wamemchambua beki huyo na kuionya Simba isimuondee na badala yake imtengenezea mazingira ya kuifaidisha timu yao.

Tangu msimu uliopita, Wawa (35) amekuwa akihusishwa kuachwa kwenye kikosi cha Simba kwa kigezo cha umri kumtupa mkono jambo ambalo lilizuiwa na aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Sven Vandenbroeck.

Sven ambaye kwa sasa anainoa FAR Rabat ya Morocco, alikuwa akiamini kuwa beki huyo bado ana mchango kwenye kikosi chake na hata baada ya kuondoka kwa Mbelgiji huyo, Wawa aliendelea kupata nafasi chini ya Didier Gomes.

Joto la kuondolewa kikosini kwa Wawa lilipamba moto zaidi kwenye mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika katika raundi ya pili dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana.

Wawa alibebeshwa lawama za kushindwa kutelekeza ipasavyo majukumu yake kama beki wa kati kiasi cha Simba ambao walikuwa na faida ya mabao mawili ambayo waliyapata kwenye mchezo wa kwanza Botswana, kutupwa nje ya michuano hiyo baada ya kukumbana na kipigo cha mabao 3-1 wakiwa nyumbani.

Kuhusiana na sakata la Wawa, Gazeti la  Mwanaspoti limewaibua mabeki wa kati wa zamani na kumzungumzia staa huyo ambaye kwa mara ya kwanza kucheza soka nchini ilikuwa 2014 akiwa na kikosi cha Azam.

Kocha wa timu za vijana wa Yanga, Bakari Malima alisema Wawa amefanya kila kitu anachostahili kufanya beki wa kati na kupewa heshima ya kuitwa mchezaji wa kigeni mwenye mafunzo makubwa dhidi ya wazawa.

SOMA NA HII  KUELEKEA KARIAKOO DABI...PABLO BAADA YA KUITAZAMA SIMBA YAKE..AGUNA KISHA ATOA KISINGIZIO...

Alisema kila anapoangalia uchezaji wake anamkumbusha beki wa kati waliowahi kucheza naye Yanga, Costantine Kimanda, raia wa Burundi anayeishi Ubelgiji kwa sasa.

“Simba wakimuacha Wawa kwa kukurupuka bila kupata mbadala wake, watajutia uamuzi wao, hata wakija kupata mbadala wake wanapaswa kumuaga kwa heshima kutokana na kile alichokifanya kwenye soka la Tanzania kwa kuleta chachu ya ufundi mkubwa alionao;

“Ni kweli kasi yake imepungua, ila waige mfano wa Yanga, walivyoachana na Haruna Niyonzima, walihakikisha wamepatikana kina Feisal Salum ‘Fei Toto’, Bangala ambao wameziba pengo lake na huoni cha kujilaumu, ila Simba bado sijaona wa kuvaa viatu vyake hadi sasa,” alisema.

Alisema pamoja na umri wake kuelekea jioni, jambo jingine analoliona Wawa linampunguza kasi ni kucheza mechi nyingi zinazomletea uchovu, hivyo kocha anapaswa kumpumzisha na kumpunguzia majukumu ili mwili wake ukae sawa.

Aliyekuwa beki wa timu hiyo na Yanga, Godwin Aswile ‘Scania’ alisema japokuwa Wawa ana akili ya mpira, kinachomkwamisha ni umri unaomfanya mwili wake kushindwa kuwajibika na kupungua kwa kasi.

Alisema wakati Wawa yupo Azam FC, alikuwa mjanja wa kumsoma straika kabla ya kumfikia katika eneo lake, ila kwa sasa mambo yamebadilika, ambapo anashindwa kufanya baadhi ya majukumu kama kugeuka kwa haraka na kuruka kwa wakati, kuokoa mipira ya juu.

“Simba waachane na Wawa kwa heshima, ili apishe wengine kama Kennedy Juma, Henock Inonga na Joash Onyango ambao miili yao ipo tayari kwa kazi, ingawa hajaisha kabisa ufundi wake kama kupiga pasi za macho na ndefu kwa usahihi,” alisema.

Mtazamo wa Aswile unatofautiana kidogo na beki mwingine wa zamani wa timu hiyo, Boniface Pawasa aliyesema Simba bado inamhitaji Wawa isipokuwa kocha, Pablo Franco ampunguzie majukumu, kutokana na umri wake hauwezi kustahimili dakika 90. “Ni kweli kasi ya Wawa imepungua, umri unaweza kuwa sababu pia fatiki inachangia.”