Home news KWA KOCHA MHISPANIA WA SIMBA…MKUDE, BOCCO NA AJIBU WASHINDWE WENYEWE TU…MRWANDA AWAPA...

KWA KOCHA MHISPANIA WA SIMBA…MKUDE, BOCCO NA AJIBU WASHINDWE WENYEWE TU…MRWANDA AWAPA NENO…

 


KOCHA wa Simba, Mhispania Pablo Franco ameleta mapinduzi ndani ya kikosi hicho ambayo yatawasaidia mastaa kushindana na kujenga timu imara na yenye ushindani.

Tangu Pablo akabidhiwe majukumu ya kuinoa timu hiyo, kuna mabadiliko katika kikosi cha kwanza, zimeongezeka sura mpya, tofauti na msimu ulioisha.

Mabadiliko hayo, yamechambuliwa na wadau wa soka, huku yakitajwa baadhi ya majina ya mastaa wa timu hiyo, kutumia fursa vyema ya Pablo wakati anatengeneza kikosi chake cha kwanza.

Staa wa zamani wa timu hiyo, Danny Mrwanda anayekipiga Ken Gold alisema kila kocha anakuja na mfumo wake, unaompa nafasi kila mchezaji kuonyesha kipaji chake.

“Nawaona Jonas Mkude, Ibrahim Ajibu, Meddie Kagere, Michael Gadiel na wengine wengi ambao msimu uliopita hawakuwa kikosi cha kwanza na sasa wanapewa nafasi, hiyo ni fursa kubwa kwao,” alisema Mrwanda na akaongeza kuwa;

“Mfano Kapombe, Shabalala walikuwa panga pangua, wakati mwingine wakiumia unaona kabisa pengo lao, Pablo anaonekana kuja kulirekebisha hilo ndio maana mechi na Red Arrows nafasi ya Kapombe alipangwa Patrick Mwenda na amefanya vizuri,” alisema.

Kauli yake iliungwa mkono na staa mwingine wa zamani wa timu hiyo, Emmanuel Gabriel ambaye ni Meneja wa Mbeya Kwanza kwa sasa, alisema kuna mabadiliko ndani ya kikosi hicho, anayoamini ni chachu ya ushindani.

“Katika nafasi moja kunapokuwa na ushindani mkali, inasaidia timu kuwa imara anayeingia na kutoka wote wanakuwa na uwezo wa kuleta matokeo,” alisema Gabriel na akaongeza kuwa;

“Kila kocha ana jicho lake la kuona nani afanye nini, wanaopewa fursa kwa sasa waikomalie wasiishi kwa mazoea kwasababu ya majina yao kuwa makubwa, lazima wafanye kazi ya kuisaidia timu na uwezo wao utapimwa uwanjani,” alisema.

Naye Said Bahanuzi straika wa zamani wa Yanga, alisema mabadiliko ya makocha mara nyingi yanawapandisha baadhi ya wachezaji na wengine kushuka.

“Mfano mzuri pale Simba, John Bocco alikuwa anaanza, sasa anaonekana kusubiri mbele ya Kagere, haina maana kwamba Bocco ni mbaya na ndiye kioo cha mastraika wa ndani, hii inatafsiri lazima kila mchezaji ajitume kwa nguvu zake zote,”alisema.

SOMA NA HII  MAMILIONI YA GSM YAZUA UTATA SIMBA..., YANGA YAWAWAHI SIMBA KWA AUCHO...MWANASPOTI LEO...

Alimzungumzia Ajibu kwamba tayari kocha ameanza kumwamini na kumpa nafasi ya kucheza, anaamini akikaza buti ataacha alama ya heshima msimu huu.

“Msimu ulioisha Ajibu alikuwa hajapata nafasi, kadri msimu huu anavyopata dakika za kucheza zitamrejesha kwenye mstari hadi atakuwa anatumika timu ya Stars,” alisema staa huyo na kukiri ligi ya msimu huu ina ushindani mkubwa.