Home news USAJILI DIRISHA DOGO…CHAMA , OKWI KURUDI SIMBA…YANGA KUACHANA NA MAKAMBO..SAMATTA AFUNGUKA…

USAJILI DIRISHA DOGO…CHAMA , OKWI KURUDI SIMBA…YANGA KUACHANA NA MAKAMBO..SAMATTA AFUNGUKA…


DIRISHA dogo la usajili nchini Tanzania linafunguliwa jana. Ndani ya mwezi huo mmoja wa kusajili lolote linaweza kutokea ikiwemo staa Clatous Chama kutua Simba au Yanga akitokea Berkane ya Morocco.

Chama ambaye hana wakati mzuri kwenye klabu yake amekuwa akihusishwa na klabu hizo hata kabla usajili haujafunguliwa na amekuwa akisisitiza kwamba ; “Muda utaongea, tusubiri tuone.”

Emmanuel Okwi wa Rayons Sports ya Rwanda amekuwa akihusishwa pia na kurejea Simba. Wapo mastaa kama Serge Wawa anahusishwa kutemwa Simba kama ilivyo kwa Heritier Makambo aliyechemka Yanga. Yote kwa yote ni kuanzia jana mpaka Januari 15.

Kipa wa zamani wa Simba, Amani Simba yeye alisema upande wa timu yake hauna sababu ya kukaa na wachezaji wa kigeni ambao wanakosa nafasi ya kucheza na pia hakuna haja ya kusajili nyota wote 12 wa kigeni bila sababu za msingi.

Kipa huyo aliwataja mastaa Peter Banda, Ousmane Sakho, Kanoute na Duncan Nyoni kuwa hakuna haja ya kuendelea nao wakati wa dirisha dogo badala yake wasajili nyota wenye ushindani zaidi.

“Simba ilipofikia siyo ya kusajili wachezaji wa kigeni wanaokaa jukwaani, wasajiliwe mafundi watano watakaoingia moja kwa moja kikosi cha kwanza, wakifanya hivyo naamini watatetea taji la ubingwa kwa mara nyingine msimu huu.

“Sioni sababu ya kujaza nafasi zote za wachezaji wa kigeni huku wengine wakiishia jukwaani, waletwe wale wanaoingia moja kwa moja kikosi cha kwanza na wengine wakali wakae benchi ila nao wawe na uwezo mkubwa,” alisema.

Kwa upande wa Beki wa zamani wa Yanga, Bakari Malima alisema wachezaji wengi wa Simba wana fataki kutokana na kucheza mechi nyingi, hivyo alishauri wapumzishwe na kupewa nafasi chipukizi.

“Tatizo tuna haraka ya mambo, Simba ina timu nzuri, wapumzishwe waliokuwa panga pangua kama Shomary Kapombe, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, wakirejea watakuwa imara na wasajili mawinga wawili,” alisema Malima na akaongeza kuwa;

“Yanga ipo vizuri lakini waboreshe kwa kuongeza winga mmoja mwenye kasi na mshambuliaji atakayewapa changamoto Fiston Mayele na Heritier Makambo,”alisema.

SOMA NA HII  MUDA WA KUKUSANYA MAOKOTO HUU HAPA...PANGA MKEKA WAKO KAMA HIVI KISHA NISHUKURU BAADAYE...

Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Makumbi Juma alisema timu hiyo inahitaji iongeza straika mmoja wa kusaidiana na Mayele, pia mfumo ubadilishwe ili kupata mabao mengi.

“Timu haiwezi kumtegemea straika mmoja tu, pia ule mfumo wa kumsimamishe mmoja mbele unawanyima mabao, kwani pasi nyingi bila pointi tatu na mabao ni bure,” alisema.

Mchezaji wa zamani wa Simba, Ally Pazi Samatta alisema timu hiyo na Yanga hawana haja ya kusajili mastaa wapya, badala yake makocha wajifunze namna ya kuwatumia waliopo.

“Mfano mzuri Aishi Manula ni miongoni mwa makipa bora Afrika, huwa nashangaa hata mechi za kawaida ambazo anapaswa kupewa Beno Kakolanya anapangwa yeye, hayo ni matumizi mabaya ya mchezaji,”alisema Samatta na akaongeza kuwa;

“Simba na Yanga zina ulafi wa kutaka kila mchezaji na hawawezi kuwatumia vizuri, ndio maana ndani ya vikosi hivyo sioni sababu ya kuondoa ama kuongeza wengine, mfano kama Paferct Chikwende walimsajili wa nini, ushauri wangu makocha wajue namna ya kuwatumia mastaa wao,” alisema.