Home Makala YAMEFICHUKA ..NI KUHUSU UDHAMINI WA GSM KWA LIGI KUU…KUMBE NI MCHEZO MREFU…

YAMEFICHUKA ..NI KUHUSU UDHAMINI WA GSM KWA LIGI KUU…KUMBE NI MCHEZO MREFU…


Mtume Muhammad (SAW) anasema ubawa mmoja wa inzi una maradhi, mwingine una dawa. Kwa hiyo inzi akitua kwenye glasi yako ya maziwa usiyamwage…mtoe, endelea kuyanywa kwa amani.

Licha ya kuwa inzi hueneza maradhi, lakini pia dawa ya maradhi hayo anayo yeye mwenyewe. Bahati mbaya tu ni kwamba watu hujikuta wamekunywa maziwa ya upande wa bawa la maradhi, halafu wakishtuka wanayamwaga maziwa kabla ya kunywa upande wa bawa lenye dawa.

Sakata la mdhamini mwenza wa Ligi Kuu Bara nalifananisha na inzi huyu. Ubawa wa maradhi ni upande wa mgogoro, lakini kuna ubawa wa dawa ambao ndiyo nataka tujadili hapa.

Hata kabla ya kusainiwa kwa mkataba huu kulikuwa na vita vya chinichini dhidi ya udhamini wa kampuni hiyohiyo kwenye klabu nyingine za Ligi Kuu. Kabla halijapoa huko, ukasainiwa mkataba na TFF. Hapo ndipo moto wa makaa ya mawe ukawaka.

Mambo mengi mabaya kuhusu mkataba huu, yaani ubawa wenye maradhi yameshasemwa na wale wanaoupinga. Sitaki hapa kuyarudia. Ila nataka kujadili mambo mazuri, yaani ubawa wenye dawa – ambayo tunaweza kuyapata endapo tunaumizwa vichwa kupitia sakata hili.

KESHO YA TPLB

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) inafanya kazi kama idara ya TFF, jambo ambalo siyo malengo ya kuanzishwa kwake.

Watendaji wa Bodi ya Ligi wanaoendeshwa na TFF, ndiyo maana unaona Boniface Wambura anatoka TFF anaenda Bodi ya Ligi halafu anarudi TFF kama mtumishi anayehamishwa kituo cha kazi. Hii siyo sawa.

Bodi ya Ligi inapaswa kuwa taasisi huru ambayo inaajiri watendaji wake kwa mikakati yake yenyewe. Inapaswa kuwa na nguvu ya kusema ‘HAPANA’ kwa TFF pale inapoona kuna jambo siyo sawa kutoka pale Karume. Na hii ndiyo Bodi ya Ligi aliyoiacha Leodegar Tenga chini ya mtendaji wake mkuu Silas Mwakibinga.

Lakini ulipoingia madarakani uongozi uliofuata 2013, ukaanza kuiingilia Bodi ya Ligi kiuendeshaji. Kwanza ulitaka kupewa pesa za udhamini, Sh100 milioni za Hanga ambazo walizikataa kutoka Azam TV. Mwakibinga aligoma hilo. Baadaye likaja suala la TFF kutaka kukopa pesa wanavyotaka kutoka Bodi ya Ligi, Mwakibinga akawa kikwazo.

Sakata la mwisho ni lile la uongozi huo kutaka TFF ipewe asilimia tano ya pesa kutoka kila mkataba wa udhamini ambao klabu binafsi itaupata. Mwakibinga kama mtendaji mkuu wa chombo cha klabu, TPLB, akalipinga hili na kumuajiri wakili msomi Damas Ndumbaro kuzitetea klabu.

SOMA NA HII  HUU HAPA NDIO USAJILI UTAKAOSUMBUA ZAIDI LIGI KUU IKIANZA...BIGIRIMANA, PHIRI, AZIZ KI NA OKRAH WOTE NDANI....

Ndumbaro akawa kikwazo kwa TFF, akafungiwa miaka sa kujihusisha na masuala ya mpira wa miguu na Mwakibinga akaondolewa. TFF ilikaribia kuivunja Bodi ya Ligi na kurudisha shughuli za usimamizi wa ligi kwa sekretarieti, lakini nadhani wakashauriwa kitaalamu kwamba hiyo italeta mgogoro mkubwa, wakaacha.

Bodi ya Ligi ya wakati ule ilikuwa inajiendesha kama chombo huru na TFF kama mmoja wa wadau wake siyo bosi wake tofauti na sasa. Nadhani kupitia sakata hili tunaweza kurudi kule na kuhakikisha tunakuwa na Bodi ya Ligi ambayo itakataa kuendeshwa.

Endapo Almasi Kisongo angesimama imara na kukataa TFF kusaini mkataba huu ili asaini yeye kama mtendaji mkuu, haya yote yasingetokea. Kwa sababu angewajibika kwa klabu ambazo ndizo zimemuajiri na angewapelekea pendekezo la mkataba walipitie na hatimaye kufikia muafaka.

Klabu zinataka kushirikishwa kwa sababu zenyewe ndizo zinazocheza ligi. Hazitaki kugeuzwa punda kwa kubebeshwa mzigo ambao hawaujui una nini ndani.

MWENYEJI KUWA NA MAMLAKA ZAIDI

Kuzuiwa kwa mtendaji mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez na familia yake kuingia uwanjani siku ya mchezo wa Simba na Yanga, kumeibua mengi. Mojawapo ni kauli ya mtendaji mkuu wa zamani wa Simba, Crencentius Magori, ambaye aliandika kupitia ukurasa wake wa Instagram akitoa wito kwa mwenyekiti wa Bodi ya Simba, mwenyekiti wa klabu ya Simba na mwanahisa mkuu kuhakikisha wanajenga uwanja wao pale Bunju halafu waone nani atawapangia cha kufanya au watu wa kuingia.

Hii tafsiri yake ni moja tu, klabu hazina mamlaka ya kutosha ya mechi zao za nyumbani. Yaani timu iko nyumbani inapangiwa bei ya viingilio, inapangiwa watu wa kuingia na hata nani wa kumualika. Hii siyo sawa hata kidogo. Timu zenyewe ziachiwe mechi zake ziendeshe wenyewe.

Zifanye promosheni, zipange bei, ziuze tiketi na ziamue nani aingie na nani asiingie – ni mechi zake. Mechi (matchday) ni bidhaa ya timu kama bidhaa zingine ambazo klabu inauza. Lakini kutokana na kuhodhiwa na mamlaka, timu hazijui kama zinaweza kuitumia siku ya mechi kutengeneza pesa zaidi ya zinazopata sasa.

Tuutumie mgogoro huu kama ufunguo wa kuingia nyumba ya ahadi. Tusiutumie kutengeneza chuki baina na yetu. Mungu ibariki Tanzania.

Makala haya yaliandikwa na kuchapiswa kwanza kwenye wavuti la Mwanaspoti.