Home news PAMOJA NA KUWA NA MASTAA WENGI WA LIGI KUU…TIMU MATAJIRI DARAJA LA...

PAMOJA NA KUWA NA MASTAA WENGI WA LIGI KUU…TIMU MATAJIRI DARAJA LA KWANZA ‘WATIWA KIMOJA’


TIMU ya Mbao imefanikiwa kutinga hatua ya 32 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) baada ya kuichapa DTB ya kwa bao 1-0.

Mchezo huo wa hatua ya nne (64 bora) umepigwa leo katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ukichezeshwa na Mwamuzi Shomari Lawi kutoka Kigoma.

Mbao imesonga mbele kibabe ikiwa timu ya kwanza msimu huu kuifunga DTB kwenye mashindano rasmi kwani DTB ambao ni vinara wa Ligi ya Championship hawajapoteza mchezo katika mechi 10 walizocheza.

Mchezo huo ulianza kwa kasi wageni wakiongozwa na wakongwe Amissi Tambwe na Nicolas Gyan walitengeneza mashambulizi lakini ngome ya Mbao ilikaa imara na kudhibiti hatari zote.

Katika dakika ya 30 Tambwe alifunga bao lakini lilikataliwa na Mwamuzi Shomari Lawi kuwa aliotea huku timu hiyo ikilazimika kufanya mabadiliko ya mapema mnamo dakika ya 43 akiingia Chunga Eliezer kuchukua nafasi ya Johnson Clement.

Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa suluhu ambapo kipindi cha pili Mbao ilibadilika na kucheza soka la kuvutia wakishangiliwa na mashabiki waliojitokeza uwanjani hapo na kufanikiwa kupata bao pekee na la ushindi mnamo dakika ya 57 likifungwa na Nassir Bitebo.

Bao hili liliwachangamsha Mbao ambao walianza kujiamini na kutengeneza mashambulizi huku DTB wakihaha kutafuta bao la kusawazisha lakini matokeo hayakubadilika.

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI YA FAINAL KESHO...MBAPPE AOMBA MSAADA WA AFRIKA KUISHINDA ARGENTINA...