Home news WAKATI YANGA WAKIENDELEA KUJITAFAKARI KISA SARE YA DABI…..SIMBA WAOGELEA MIHELA…

WAKATI YANGA WAKIENDELEA KUJITAFAKARI KISA SARE YA DABI…..SIMBA WAOGELEA MIHELA…


KUNA watu wamefuraahi kupata sare pale Kwa Mkapa juzi, lakini kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi amewatuliza mashabiki wa timu yake akisema dhamira yao ya kutwaa ubingwa na mataji yote msimu huu yako palepale.

Yanga walitoka sare ya 0-0 dhidi ya Simba juzi katika mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu Bara msimu huu,matokeo ambayo hayakutarajiwa na wengi hasa baada ya Wekundu wa Msimbazi kupoteza 1-0 mechi ya ufunguzi wa msimu ya Ngao ya Jamii, ambayo waliusaka mpira kwa tochi.

Lakini juzi, Simba ilikuwa bora huku beki wao, Inonga Baka, akisifiwa kwa kumtia mfukoni straika wa Yanga Mcongo mwenzake aliyeamua mechi iliyotangulia, Fiston Mayele.

Baada ya mechi ya juzi, Nabi alimpongeza kocha wa Simba, Pablo Franco, akisema amefanya kazi kubwa ya kukitengeneza kikosi chake ambacho kimeimarika zaidi, jambo ambalo alilisema hata kabla ya mchezo huo kuwa utakuwa 50/50 na kweli ilikuwa hivyo.

Nabi amecheza dabi nne za Kariakoo chini ya makocha watatu, Sven Vandenbroeck, Didier Gomes na Pablo na kwamba kikosi cha jana kilionyesha kuimarika sana.

Alisema katika mechi hiyo Yanga walicheza vizuri zaidi katika kipindi cha kwanza na kutengeneza nafasi nne za kufunga ila walishindwa kuzitumia kutokana na wachezaji wake kukosa umakini.

“Kipindi cha pili mechi ilibadilika kwa Simba kucheza vizuri ingawa wao walitengeneza nafasi moja tu ya kufunga ile dakika za mwisho baada ya Djugui Diarra kucheza shuti kali lililopigwa (na Sadio Kanoute),” alisema Nabi na kuongeza;

“Naendelea kuboresha kikosi cha Yanga kuwa imara zaidi ya sasa ili tuache kufanya makosa ya mara kwa mara kama yale ya kushindwa kutumia nafasi za kufunga kama ile aliyokosa Said Ntibazonkiza.”

Kocha wa Simba, Pablo aliipongeza timu yake na wachezaji kutokana na kazi nzuri waliyoifanya kulingana na mpango yao ya mechi dhidi ya Yanga.

Pablo alisema ilikuwa mechi yenye kuhitaji mbinu nyingi zaidi ndio maana hapakuwa na nafasi za kutosha kufunga kwa timu zote mbili na si rahisi kucheza na kutawala mechi wakati wote katika mchezo mkubwa kama huo.

SOMA NA HII  HUYU HAPA MCHEZAJI MTZ ANAYETIKISA ULAYA ...KOCHA TAIFA STARS KUMUITA KIKOSINI...

SIMBA MIJIHELA

Uongozi wa Simba umeonekana kuridhishwa na juhudi zilizofanywa na wachezaji wake katika sare ya 0-0 dhidi ya Yanga na hivyo kuwajaza mamilioni nyota hao.

Sio kawaida kwa timu hiyo kuwapa pesa wachezaji wake wakipata sare, lakini kutokana na kuingia katika mechi ya juzi wakitokea kufungwa 1-0 katika dabi yao iliyotangulia ambayo pia walipigiwa mpira mwingi, uongozi umeonyesha kufurahishwa na juhudi za wachezaji waliopambana kishujaa.

Nyota wa Simba siku moja kabla ya mechi waliambiwa na kama watashinda mechi hiyo watachukua Sh200 milioni kama bonasi ila wakitoka sare watapewa Sh100 milioni.