Home Simba SC KATI YA KAHATA NA CHIKWENDE, MMOJA KUPUNGUZWA SIMBA SC

KATI YA KAHATA NA CHIKWENDE, MMOJA KUPUNGUZWA SIMBA SC


MWISHO wa msimu huu benchi la ufundi la Simba lililokuwa chini ya kocha Didier Gomes pamoja na uongozi wa timu hiyo utakuwa na uamuzi mgumu dhidi ya nyota wake wawili.

Nyota hao ni Mkenya Francis Kahata anayecheza Ligi ya Mabingwa Afrika na Mzimbabwe Perfect Chikwende anayeupiga mashindano ya ndani.

Mwisho wa msimu huu, Simba watalazimika kumuacha mchezaji mmoja wa kigeni ili kubaki nao 10, huku Kahata ambaye alishaonekana kuna dalili ya kutoka amekuwa kipenzi cha Gomes na huenda akatamani kuwa naye msimu ujao, jambo linaloweza kumuweka hatarini Chikwende.

Ufuatao ni uchambuzi wa Kahata katika mechi sita za Ligi ya Mabingwa ambazo amecheza pamoja na Chikwende mechi 11 za mashindano ya ndani ambazo ametumika.

Tangu kusajiliwa kwa Chikwende, Kahata amecheza mechi zote sita katika hatua ya makundi huku akitumia dakika 100, akiwa hajafunga bao, lakini amehusika katika shambulizi ambalo Simba walipata bao la pekee dhidi ya AS Vita walipokuwa ugenini DR Congo.


Katika mechi ya AS Vita aliingia dakika 60 akichukua nafasi ya Rarry Bwalya na dakika moja baadaye alihusika katika bao la Chriss Mugalu. Mechi na Al Ahly aliingia dakika ya 87 akichukua nafasi ya mfungaji wa bao, Luis Miquissone.

Kwenye mechi ya ugenini dhidi ya Al Merrikh aliingia dakika 77 akichukua nafasi ya Clatous Chama wakati mechi ya marudiano na timu hiyo aliingia katika dakika 83 nafasi ya Luis Miquissone mfungaji wa bao la kwanza.

Kahata, katika mechi na AS Vita aliingia dakika 87 akichukua nafasi ya Miquissone ambaye alifunga bao la kwanza dakika 30, wakati mchezo wa mwisho hatua ya makundi dhidi ya Al Ahly aliingia dakika 46 akimrithi Bwalya.

Kutokana na rekodi hizo,  Kahata amesema kazi yake ni kucheza mechi ambazo atapewa nafasi ya kuitumikia timu yake.

Kahata anasema jukumu lake ni kuitumikia Simba ili ipate mafanikio bila kujali ni katika mashindano ya aina gani au anatumika muda gani.

“Kuhusu mkataba wangu kumalizika hilo sidhani kama huu ni muda sahihi wa kulizungumzia, ambacho nahitaji ni kuitumikia Simba kadri ambayo nitaweza ili kuipa mafanikio kutokana na malengo ambayo tumejipangia na baada ya hapo mengine yatafuata,” anasema Kahata.

SOMA NA HII  CHE MALONE:- NATAKA CHANGAMOTO MPYA...HUENDA MSIMU UJAO NIKACHEZA TIMU KUBWA ZAIDI...

Kwa upande wake, Chikwende alisajiliwa na Simba akitokea FC Platinum ya Zimbabwe na Januari 15, mwaka huu alitambulishwa kama mchezaji halali wa timu hiyo ila atatumika katika mashindano ya ndani.

Mechi yake ya kwanza ya kimashindano kucheza ilikuwa Februari 4 – mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji alioingia dakika 61 akichukua nafasi ya Miquiossone.


Katika mechi hiyo Simba walishinda mabao 2-1 ugenini na Chikwende alitoa pasi ya mwisho kwa Bernard Morrison aliyefunga bao la ushindi dakika 66.

Mechi iliyofuata ilikuwa dhidi ya Azam alianza katika kikosi cha kwanza na alitolewa dakika 70 na kuingia Chriss Mugalu. Alicheza dakika zote katika mechi na Biashara United.

Chikwende alianza katika mechi na Tanzania Prisons na alitolewa dakika ya 50, huku mechi iliyofuata dhidi ya Mtibwa aliingia na kucheza dakika 35, wakati ile na Mwadui alianza na kutolewa baada ya dakika 45.

Mzimbabwe huyo alicheza dakika zote 90 katika mechi ya Kombe la Shirikisho (ASFC), dhidi ya African Lyon na aliifungia timu yake bao la tatu baada ya Ibrahim Ajibu kufunga mawili ya awali.

Chikwende pia hajatumika katika mechi nne ambazo Simba walishinda zote dhidi ya JKT Tanzania, Kagera Sugar, Gwambina na Dodoma Jiji. Rekodi zinaonyesha Chikwende amecheza mechi saba, dakika 409 na kufunga bao moja katika mchezo wa ASFC, huku akitoa pasi ya mwisho katika mechi ya ligi dhidi ya Dodoma Jiji ugenini.

Kocha wa zamani wa Simba, Masoud Djuma anasema wachezaji wote ni wazuri kulingana na aina ya mechi ambayo Simba wata-kuwa wanakutana nayo.

Djuma anasema kama unataka winga ambaye anakimbia muda mwingi Chikwende anaweza kuwa sahihi, kama ambavyo kwa Kahata ambaye ni mzuri anapokuwa na mpira mguuni.

“Jukumu litabaki kwa kocha aina gani ya winga ambaye anataka kumtumia, yule mwenye ufundi zaidi mguuni au mwenye spidi za mara kwa mara,” anasema Djuma ambaye alikuwa kocha msaidizi wa Simba chini ya makocha wakuu Joseph Omog, Pierre Lechantre na Patrick Aussems.

Kwa rekodi hizo, Kahat yupo juu ya Chikwende, lakini nini kitatokea mwisho wa msimu? Ni suala la kusubiri na kuona.