Wakati timu zikiendelea kuimarisha vikosi vyao katika kipindi hiki cha dirisha dogo, Mbeya City wamemnasa Kipa wa zamani wa Yanga na Simba, Deogratias Munish ‘Dida’ kuongeza nguvu kikosini.
Dirisha dogo lilifunguliwa tangu Desemba 15, 2021 na litafungwa Januari 15 2022 ambapo timu za First League, Championship na Ligi Kuu kwa Wanaume na Wanawake wanalitumia kuboresha maeneo yenye mapungufu.
Hata hivyo Meneja wa timu hiyo, Mwagane Yeya licha ya kutothibitisha moja kwa moja, amesema huenda nyota huyo akawa miongoni mwa kikosi chao wakati wakiendelea kujiimarisha na mwendelezo wa Ligi Kuu.
Amesema wanaamini uwapo wa mkongwe huyo utaisaidi timu na kwamba matarajio yao siyo kuongeza wachezaji wengi isipokuwa hawatazidi wanne katika nafasi tofauti.
“Tunaweza kuwa naye Mungu akijaalia, tunaamini atatusaidia katika kufikia malengo, hatutarajii kuongeza wengi yaani ni wanne tu eneo la beki, kiungo na Straika basi” amesema Yeya.
Pia Meneja huyo amesema hawatarajii kuacha mchezaji yeyote badala yake wale walioshindwa kuonesha uwezo na kulishawishi benchi la ufundi watapelekwa timu nyingine kwa mkopo.
Ujio wa Kipa huyo mkongwe na mzoefu, unafikisha Makipa watatu kikosini, ikiwa ni Ibrahim Isihaka na Haroun Mandanda ambaye amekuwa namba moja ndani ya timu yao na Taifa Stars.