KOCHA wa Simba, Pablo Franco amesema licha ya kiungo Sharaf Shiboub kuwahi kuichezea Simba, anapaswa kuonesha kiwango kwenye mechi za Kombe la Mapinduzi ili kuamua hatima yake.
Amesema hayo baada ya kuonekana Shiboub anaweza kupata wepesi wa kusajiliwa kwenye kikosi hicho kwa sababu aliwahi kuitumikia timu hiyo.
Shiboub alitua katika klabu hiyo mwanzoni mwa wiki hii akiambatana na winga wa kushoto, Moukoro Tenena wa Ivory Coast kwa ajili ya majaribio na kujumuishwa kwenye kikosi kinachoshiriki Kombe la Mapinduzi.
“Ni mchezaji ambaye nimepata taarifa zake kuhusu kucheza Simba lakini simfahamu, sijawahi kumuona zaidi ya kumuona mazoezini, hivyo nitamuangalia zaidi kwenye mechi za Mapinduzi na kuamua hatima yake.”
“Lakini ukizungumzia kuhusu ushindani, timu imekuja kiushindani kwa hiyo kila mmoja anapaswa kujitoa ili nipate kipimo kamili maana hii ni michuano na wachezaji wote wanaopata nafasi nahitaji kuwaangalia zaidi hata huku nataka ushindi katika kila mechi,” alisema Pablo.
Juzi, Shiboub alicheza katika mchezo wa kwanza wa Simba wa michuano hiyo dhidi ya Selem View kwenye Uwanja wa Amaan na kuibuka na ushindi wa 2-0.
Shiboub aliwahi kuichezea Simba msimu wa 2020/21 kabla ya kuachwa baada ya mkataba wake kumalizika na Tenena anayetajwa kuichezea El Masry, Al-Hilal na ASEC Mimosas amekuja kujaribiwa.