BEKI Pascal Wawa ni kama vile ameanza kulizoea benchi baada ya kushindwa kumshawishi moja kwa moja Kocha wake, Pablo Franco ili aweze kuingia katika kikosi chake cha kwanza.
Wawa ambaye kwa misimu mitatu mfululizo amekuwa kwenye kikosi cha kwanza, lakini kwa sasa ameanza kupotea kidogo mbele ya Henock Inonga aliyetengeneza kombinesheni nzuri na mkongwe Joash Onyango.
Wadau wa soka nchini wamemtaka mchezaji huyo ajishtukie mapema kwa sababu uwezo wa kucheza kikosi cha kwanza anao lakini ni suala la yeye kuzidi kujitambua anapokuwa uwanjani.
Kocha wa zamani wa Biashara Utd, Amani Josiah alisema “Wawa ana uzito fulani na inawezekana imetokana na umri kusogea, mwalimu kaona kuna wepesi kwa wawili (Joash na Henock), sasa kukaa nje kwa Wawa haimaanishi kwamba ni mchezji mbaya,” alisema Amani.
Naye mshambuliaji wa zamani Yanga, Hery Morris alisema “Unajua ukiwa mchezaji unapoona nafasi yako kaletwa mtu mwingine inabidi ushtuke na kuendeleza moto wako na sio kuridhika, mwalimu pia amebadilika kwa hiyo inabidi ujipange vilivyo kuhakikisha unamshawishi.”
Katika mechi tisa za mwisho kwa mashindano yote ya Simba walizocheza, Wawa ameshindwa kuanza katika mechi za Ligi dhidi ya Azam,Yanga, KMC na Mbeya City huku kwenye upande wa Kombe la Mapinduzi akikosekana dhidi ya Namungo na Azam.