YANGA imefanikiwa kupigana vita kubwa kumbakisha winga wao mpya Chico Ushindi aliyekaribia kusitisha dili hilo, lakini neema ikamwangukia kiungo wao wa zamani, Mukoko Tonombe ambaye amepata mshahara wa kufuru.
Katika dili la miaka miwili ambalo Mukoko amesaini na TP Mazembe mabosi wa Yanga wametumia akili kubwa kuwakamua Wakongomani hao kuhakikisha kiungo huyo anabadili akili yake kukubali dili hilo.
Mukoko sasa atakuwa akilipwa mshahara wa Dola 8000 (Sh18.4 milioni) kwa mwezi na Mazembe pesa ambayo hakuna staa yeyote wa Yanga anaweza kuivuta katika kikosi hicho, wakati akiwa Yanga alikuwa akichukua Dola 3000 (Sh7 milioni) kwa mwezi.
Mbali na pesa hiyo, Mazembe pia wamemshawishi zaidi wakimpa kiasi cha Dola 100000 (Sh230 milioni) kama ada ya usajili katika dili hilo la miaka miwili.
Hata hivyo, Yanga nao wamepiga bao na watapewa Ushindi kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu na sio miezi sita tena kama ilivyokuwa awali.
Kocha wa Yanga, Nesreddine Nabi aliwaambia mabosi wa Yanga katika mazungumzo yao na Mazembe wahakikishe wanambakisha Ushindi kwa nguvu yoyote kwa kuwa kuna kitu kizito amekiona kwa winga huyo tangu ajiunge na wenzake.
Mazembe yafichua usajili wa Aucho
Bosi wa Mazembe, Andrea Mutini amelifichulia gazeti la Mwanaspoti Yanga iliwahi kuipa pigo zito klabu yao wakati wa usajili wa Aucho dirisha kubwa la usajili.
Mutini alisema wakati Aucho anataka kuachana na klabu yake ya nchini Misri, Mazembe walisikia habari hizo kisha kujipanga kwenda kumchukua haraka.
“Wakati tunamtuma mtu aende kumchukua Aucho kule Misri, kumbe mtu aliyetupa taarifa hakujua Aucho ameshakata tiketi ya kuja Tanzania. Sisi tulipoondoka kumfuata tukaona ameshatua Tanzania,” alisimulia Mutini ambaye ni msaidizi wa karibu wa Bilionea wa Mazembe, Moise Katumbi.
“Yule tuliyemtuma alipofika Misri akaambiwa bahati mbaya sana Aucho ameondoka saa chache zilizopita hapo ndipo Yanga walipotupiga bao, ilikuwa tumchukue.
“Nimeona hii mechi ukiacha Bangala (Yannick) huyu Aucho ni mtu bora sana, nimeumia mara mbili, anafanya kazi nyingi sana kubwa katika eneo la kiungo la Yanga,”alisema Bosi huyo.