YANGA inatamba kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 36 baada ya mechi 14 na kasi iliyonayo, wengi wameipa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu mbele ya Simba, labda itokoee miujiza tu.
Ikiwa imefikisha jumla ya mechi 21 bila kupoteza katika ligi hiyo tangu ilipolala bao 1-0 kwa Azam FC Aprili 25, mwaka jana, Yanga imekuwa ikiwapa burudani mashabiki wake, lakini nyuma ya ubabe huo imechangiwa na mastaa wake sita.
Tangu kipigo cha bao la mbali la Prince Dube, Yanga ilicheza mechi saba za msimu huo kisha kuunganisha michezo 14 za msimu huu, ikishinda 11 na kutoka sare tatu na kufunga mabao 23 na kufungwa manne na kuifanya iwe timu pekee ambao haijaonja kipigo hadi sasa.
Hata hivyo, siri ya Yanga imechangiwa na kiwango bora kinachoonyeshwa na kundi kubwa la wachezaji wa timu hiyo, huku sita kati yao wakionekana kutoa mchango mkubwa kwa kucheza kwa dakika nyingi zaidi katika ligi msimu huu.
Nyota hao ambao benchi la ufundi la Yanga chini ya Kocha Nasreddine Nabi linaonekana kuwaamini zaidi na kuwapa nafasi ya kubwa ya kucheza ni Djuma Shaban, Yannick Bangala, Dickson Job, Khalid Aucho, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Fiston Mayele ambaye ndiye kinara wa mabao wa kikosi hicho akiwa na sita.
Kinara aliyecheza dakika nyingi zaidi ni beki wa kati Dickson Job ambaye licha ya mashabiki wa timu hiyo kutomuimba sana, ndiye amewakimbiza mastaa wote wa timu hiyo kwa kuaminika zaidi na Nabi na kupangwa mara kwa mara.
Job amecheza mechi 15 mfululizo za Yanga kuanzia ile ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba na 14 zilizofuata za Ligi Kuu sawa na dakika 1,350 na katika mechi hizo zote amecheza kwa dakika 90 bila kupumzishwa.
Anayemfuatia Job kwa kucheza kwa muda wa kutosha katika kikosi cha Yanga ni beki wa kulia, Djuma aliyetumika katika timu hiyo kwa dakika 1,167 huku akiifungia mabao mawili.
Nyuma yao yupo kiungo kiraka, Bangala ambaye katika msimu huu ameitumikia Yanga kwa dakika 1,161 ikiwa ni wastani wa takribani mechi 13.
Straika tishio anayeshika nafasi ya pili kwa kufumania nyavu katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, Mayele yeye ndani ya kikosi cha Yanga anakamata nafasi ya nne kwa kucheza dakika nyingi ambapo ameitumikia kwa muda wa dakika 1,153.
Nafasi ya tano inashikiliwa na kiungo fundi wa ushambuliaji, Fei Toto aliyetumika kwa dakika 1,144 na kiungo mkabaji kutoka Uganda, Aucho anashikilia nafasi ya sita kwa kucheza dakika nyingi akitumika kwa dakika 1,059.
WASIKIE WADAU
Mchambuzi wa soka, George Ambangile alisema makocha wengi wamekuwa wakiamini zaidi kwenye kuimarisha safu ya ulinzi kutokana na kutokuwa na mabadiliko ya mara kwa mara.
“Nilitegemea kuliona hili kwasababu safu ya ulinzi huwa haifanyiwi mabadiliko mara kwa mara kutokana na kutumika sana na walinzi waliokaa pamoja muda mrefu na kuzioana tofauti na washambuliaji ambao wamekuwa wakifanyiwa mabadiliko mara kwa mara,” alisema.
Naye mchezaji wa zamani wa Yanga, Said Maulid ‘SMG’ alisema mastaa wa Yanga wameanza vizuri mzunguko wa kwanza bado wanakazi ya kufanya wache kuridhika na matokeo.
“Kocha Nabi amekuwa na wastani mzuri wa kutumia wachezaji na mbinu zake zimeonekana kuwa bora kwa wapinzani wake anahitaji kuendeleza aliyoanza nayo kwa kuongeza nguvu zaidi kwani duru la pili utakuwa mgumu timu zinahitaji pointi kama wao,” alisema.
SMG alisema anaipa nafasi kubwa Yanga kutwaa taji msimu huu kutokana na kikosi na uchu wa mafanikio kwa wachezaji ambao wanatamani kuona timu yao inakuwa bora na inatwaa mataji.
Wakati huo huo Ally Mayay alisema anaona namna wazawa pia walivyoamka kuonyesha ushindani kwa wageni huku akimtaja Job kuwa ni beki mwenye nidhamu na bora.