VIUNGO wa Yanga, Khalid Aucho na Yanick Bangala wameundiwa tume mapema na Mtibwa Sugar kuhakikisha hawaendi kusumbua kwa kutumia uzoefu wao kwenye mchezo ujao wa Ligi Kuu.
Mtibwa na Yanga zinakutana leo katika pambano litakalopigwa kwenye Uwanja wa Manungu litakaloanza saa 10:00 jioni, huku Yanga ikiwa kileleni mwa msimamo kwa pointi 36 baada ya mwechi 14, ikifunga mabao 23 hadi sasa.
Kiungo wa Mtibwa Sugar, Baraka Majogoro alisema mbinu kubwa ya kukabiliana na wachezaji hao wameambiwa kucheza nao kwa nidhamu ya hali ya juu.
Majogoro alisema wachezaji hao wana uzoefu mkubwa hivyo mwalimu wao mara kwa mara amekuwa akiwaambia wawaheshimu wapinzani na kucheza kwa nidhamu kubwa uwanjani.
“Kwanza mimi binafsi nawaheshimu wapinzani hao kwa sababu wapo kwenye timu kubwa, kikubwa tumesisitizwa kuwaheshimu na sisi tucheze mpira wetu kwa utulivu ndani ya uwanja,” alisema Majogoro.
Majogoro kwenye eneo la kiungo huwa anacheza sambamba na Said Ndemla kwenye kikosi cha Mtibwa.
Rekodi zinaonyesha Yanga hutaabika sana mbele ya Mtibwa katika mechi zinazopigwa mjini Morogoro kwani katika mechi 10 zilizopita mjini humo Yanga imeshinda mara mbili tu huku nyingine zikiwa ni vipigo ama sare.
Hii ni mara ya kwanza kwa timu hizo kukutana Manungu baada ya uwanja huo kuzuiwa na mamlaka za soka na mechi za nyumbani za Mtibwa kuhamia Jamhuri Morogoro, kabla ya safari hii kurudishwa tena Manungu.