KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, amepanga kumtumia kiungo wake, Feisal Salum ‘Fei Toto’, kama njia rahisi ya kupata ushindi dhidi ya Mtibwa Sugar, leo Jumatano katika mchezo wa Ligi Kuu Bara utakaochezwa Uwanja wa Manungu, Morogoro.
Mchezo huo ni wa kumaliza mzunguko wa kwanza ambapo Yanga ipo kileleni na alama zake 36, huku Mtibwa ikishika nafasi ya 15, ikikusanya alama 12, zote zikicheza mechi 14.
Chanzo chetu kutoka Yanga, kimesema kwamba, katika mazoezi ya kuelekea kwenye mchezo huo, Nabi ameamua kumuongezea mbinu za ufungaji Fei Toto, lengo likiwa ni kumfanya afunge wakati wapinzani wakimkaba mshambuliaji wao hatari, Fiston Mayele.
“Kocha wetu hana shaka kabisa na taarifa za ubovu wa Uwanja wa Manungu, zaidi yeye yuko bize kuhakikisha anamnoa Fei Toto katika suala la kufumania nyavu kwani mazoezi mengi ameonekana akimtaka kutumia kila nafasi kufunga.
“Hiyo ni katika kuhakikisha timu inapata ushindi kwa sababu tunafahamu kwamba wapinzani watakuwa bize kumkaba Mayele, jambo ambalo litatoa mwanya kwa wengine kufunga na kupata ushindi tunaouhitaji,” kilisema chanzo hicho.
Msimu huu katika Ligi Kuu Bara, Mayele amekuwa chachu kubwa ya ushindi kwa Yanga akiwa amefunga mabao sita, ndiye kinara wa mabao kikosini hapo, huku Fei Toto akiwa nayo manne.