Home news TFF YAWAPIGIA MAGOTI GSM…WARUDI MEZANI UPYA KUJADILI DILI..MGUTO ATUPA MPIRA KWA KIDAO..

TFF YAWAPIGIA MAGOTI GSM…WARUDI MEZANI UPYA KUJADILI DILI..MGUTO ATUPA MPIRA KWA KIDAO..


KAMA ulikuwa unadhani dili la udhamini wa Kampuni ya GSM katika Ligi Kuu Bara limekufa, pole yako kwani kampuni hiyo na Shirikisho la Soka nchini (TFF) wamerudi mezani kuujadili upya mkataba huo ili GSM iendelee kuidhamini ligi.

GSM ilitangaza kujitoa kama mdhamini mwenza wa Ligi, Februari 7 kwa madai ya kutotimizwa kwa makubaliano ya mkataba baina yao, TFF na Bodi ya Ligi (TPLB).

Uamuzi huo ulikuja zikiwa zimepita siku 76 tu, tangu waliposaini mkataba wa Sh2.1 bilioni Novemba 23, mwaka jana huku mkataba huo uliopingwa na Simba kueleza kutoutambua na kugomea kuvaa logo za udhamini huo.

Hata hivyo, juzi mmoja wa viongozi wa juu wa TFF aliyeombwa kuhifadhiwa jina lake, alidokeza kuwa, tayari wameanza mazungumzo ya kuona ni namna gani GSM atarejea kuendelea kuwa mdhamini mwenza wa Ligi Kuu.

“Kinachofayika sasa ni kuona ni namna gani changamoto zilizojitokeza zinawekwa sawa na mazungumzo yanakwenda vizuri na kuna matumaini kwa kiasi fulani wa kupata muafaka wa jambo hili ili GSM arudi Ligi Kuu,” alisema kigogo huyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mnguto alipoulizwa kuhusu mpango huo alisema suala hilo liko chini ya Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao na Mkuu wa Idara ya Habari na Masoko, Boniface Wambura.

“Kitengo cha Habari na Masoko ndicho kinasimamia mchakato wote kuona ni namna gani jambo hilo linakwisha, ndio maana hata mabango ya GSM bado hayajatolewa tukitarajia kufikia muafaka na kuendelea na udhamini huo,” alidokeza kigogo huyo wa TFF.

Mkuu wa Idara ya Habari na Masoko wa TFF, Boniface Wambura alipotafutwa kwa siku tatu mfululizo ili kutoa ufafanuzi wa taarifa hizo, simu yake iliita bila kupokewa.

Hata hivyo, taarifa ya GSM kutaka kurudi ilipokelewa kwa shangwe na baadhi ya klabu za Ligi Kuu zikieleza kufurahishwa na mkakati huo kama utafanikiwa na kusisitiza kwamba zinahitaji udhamini kwa sasa kuliko kitu chochote.

“Maisha ya klabu yetu ni magumu mno, hivyo tunapopata udhamini kutoka sehemu tofauti tofauti inatusaidia kwa kiasi kikubwa,” alisema mwenyekiti wa moja ya klabu hizo.

SOMA NA HII  KUELEKEA MSIMU UJAO...AZAM WATAKA KUFANANA NA SIMBA KILA KITU...NAO WAPANGA KUIFUATA AL AHLY...