Baraza la Michezo Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), inajipanga kuboresha mashindano yake yote hili kuwa na nguvu na kurudisha ushindani uliopo kama zamani.
Akizungumzia katika mkutano wa Baraza hilo ambalo limefanyika leo Februari 25, jijini Arusha, Mwenyekiti wa Cecafa ambaye pia ni Raisi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema watahakikisha kila mwanachama yanapotekea mashindano ya timu za taifa wanashiriki lakini pia wanapanga kuweka sheria kali ambazo zitafanya klabu kushiriki mashindano na siyo kujiondoa.
Ameongeza kuwa wamejipanga kuyapa nguvu mashindano yote yatakayao andaliwa na CECAFA pia wanatarajia kuwasiliana na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na shirikisho la mpira wa miguu Duniani (FIFA), kuhakikisha wanatumia sheria zao na utaratibu unaoeleweka.
“Mashindano bila kuwa na nguvu hatuwezi kupata wadhamini tutahakikisha kwamba wanachama wote inapotokea mashindano yanayohusu timu za taifa wanashiriki wote pia tutaweka sheria kali ambazo zitafanya kila klabu kushiriki siyo zingine kujiamulia kujitoa kwenye mashindano” amesema Karia
Kwa upande wa mchambuzi wa soka ,Ibrahim Masoud “Maestro” amesema mwitikio umekuwa mkubwa wanachama kushiriki mkutano huo kutokana na kuwa na imani ya uongozi uliopo wasasa chini ya Mwenyekiti wake Wallace Karia na wameona ni fursa ya kujua wapi walikwama na nini wanapaswa kufanya.
Mkutano huo ni wakwanza kufanyika tangu uongozi mpya kuingia madarakani chini ya Karia ambao ulikuwa na ajenda mbalimbali zikiwemo taarifa za hesabu za fedha za shirikisho ambayo haikumalizika na watajadiliana baada ya miezi mitatu, pia ajenda nyingine ni kuhusiana na mashindano mbalimbali ambayo yatafanyika mwaka huu katika ngazi tofauti tofauti.