Home news KUELEKEA MECHI YA SHIRIKISHO CAF…BWALYA NA SAKHO WATAJWA WACHEZAJI BORA…KOCHA WA ASEC...

KUELEKEA MECHI YA SHIRIKISHO CAF…BWALYA NA SAKHO WATAJWA WACHEZAJI BORA…KOCHA WA ASEC AOGOPA…


BAADA ya kukitazama kikosi cha Simba, Kocha Mkuu wa Asec Mimosas ya nchini Ivory Coast, Julien Chevalier, amewataja wachezaji Pape Ousmane Sakho na Rally Bwalya kuwa ni wa kuchungwa kutokana na ubora walionao, hivyo wanajiandaa kuwadhibiti kwa vyovyote vile wasilete madhara kwao.

Asec Mimosas wanatarajiwa kuwa wageni wa Simba katika mchezo wa kwanza wa Kundi D kwenye Kombe la Shirikisho Afrika utakaochezwa Februari 13, mwaka huu, Uwanja wa Mkapa, Dar. Katika kundi hilo, timu zingine zilizopo ni RS Berkane ya Morocco na Union Sportive Gerndamarie ya nchini Niger.

Akizungumzia juu ya maandalizi yao kuelekea mchezo huo, kocha huyo amesema wanapokwenda kucheza dhidi ya Simba, Sakho na Bwalya ni wachezaji wa kuchungwa kutokana na kuwa na madhara makubwa kwa wapinzani, pia wana uwezo mzuri wa kumiliki mpira.

“Simba nimewafuatilia katika baadhi ya michezo yao, wana timu nzuri na wachezaji wengi wazuri, siwezi kuwataja wote, lakini kuna kiungo wa kati Bwalya na winga Sakho, ni wachezaji wazuri.

“Ni wachezaji ambao hata sisi tunatakiwa kuwachunga kutokana na uwezo wao kwa jinsi ambavyo nimeitazama Simba, wanaweza kukokota mpira na kumiliki pia, tutafanya kile kilichobora kupata matokeo mazuri dhidi yao,” alisema kocha huyo.

Naye Meneja wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema  kwamba: “Tunajua hauwezi kuwa mchezo rahisi kwetu kwa sababu tunacheza nyumbani, hii ni michuano mikubwa na inashirikisha timu bora, hivyo ni wazi tunatarajia mchezo mgumu na tumejiandaa vizuri.

“Kocha amepata muda wa kuwasoma wapinzani wetu na malengo yetu makubwa ni kutumia faida ya kucheza kwenye uwanja wa nyumbani kupata matokeo mazuri.

“Tunataka kufuzu robo fainali na hesabu zetu ni kushinda mechi zote za nyumbani ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kufikia malengo.”

SOMA NA HII  MUONEKANO WA LAKE TANGANYIKA, DIMBA LA FAINALI FA