Home news WAKATI WENZAKE WAKIJIANDAA KUINGIA UWANJANI..HIVI NDIVYO CHAMA ALIVYOUZA RAMANI KWA SIMBA…

WAKATI WENZAKE WAKIJIANDAA KUINGIA UWANJANI..HIVI NDIVYO CHAMA ALIVYOUZA RAMANI KWA SIMBA…


SIMBA ipo katika mji wa Berkane tayari kwa mechi yao dhidi ya RS Berkane, huku kiungo fundi wa mpira ambaye hata hivyo hatatumika kwenye mchezo huo, Clatous Chama akiuza ramani ya vita ya Wamorocco, huku akiwajaza upepo mastaa wenzake akiwaambia wapinzani wao wanafungika kabisa licha ya kucheza nyumbani.

Kiungo huyo alisajiliwa na RS Berkane Julai mwaka jana mara baada ya kuisaidia Simba kutetea ubingwa wa Ligi Kuu kwa msimu wa nne mfululizo na Kombe la ASFC kwa misimu miwili mfululizo kisha kukaa na wababe hao wa Morocco hadi kwenye dirisha dogo la usajili la msimu huu lililofungwa Januari 15 kabla ya kurejea tena Msimbazi.

Kutokana na kuwepo kwenye orodha ya usajili wa CAF ya Berkane, Chama anabanwa na kanuni za michuano ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kuitumikia Simba, lakini hiyo haijamzuia Mzambia huyo kuichoma tmu yake ya zamani kwa mabosi wake wa sasa.

Kiungo huyo ameambatana na timu hiyo kwenye safari ya ugenini ya mechi za Kundi D ya Kombe la Shirikisho dhidi ya USGN na hiyo ya kesho dhidi ya Berkne kwa kazi maalumu ya kuuza siri za Wamorocco, lakini pia akitumika kuwajaza hamasa mastaa wenzake waliotoka kupata sare ya 1-1 mjini Niamey, Niger.

Akizungumza  kutoka Morocco, Chama alisema tangu atue kwenye timu hiyo na wakati wa mechi hizi za kimataifa amekuwa akitumika kama mhamasihaji wa wenzake, sambamba na kulisaidia benchi la ufundi kuwapa mchoro mzima wa kuimaliza Berkane.

Chama alisema alikutana na wachezaji wenzake katika kambi yao iliyopo Casablanca kabla ya kuhamia Berkane jana Ijumaa, akiwahamasisha kila mmoja ambaye atapata nafasi ya kucheza kupambana vya kutosha katika kutimiza majukumu yake uwanjani na pia akilisaidia pia benchi lao la ufundi.

Alisema ametoka huko huko Morocco katika timu hiyo ya Berkane ni wazi kuna vitu atakuwa anavifahamu kutoka kwa wapinzani wao na amewaeleza wachezaji wenzake namna gani wataweza kwenda kuvitumia na kupata wanachokihitaji mwisho wa mchezo.

SOMA NA HII  EHEEEH....HUYU KAPOMBE KASHINDIKANA AISEEE...MAMBO ALIYOYAFANYA NI ZAIDI YA 'CONNECTION'...

“Hata benchi la ufundi kwa awamu tofauti waliniuliza kuhusu mambo fulani ya wapinzani wetu pamoja na huku Morocco nimewapatia na nina iimani tutakwenda kupata matokeo mengine bora ugenini,” alisema Chama na kuongeza;

“Wapinzani ni wazuri tumeambiana hilo kama ambavyo kwenye sehemu ambazo wana shida na yote haya yanafanyika ili kuona tunafanikiwa na kuendelea kuongoza kundi,

“Kila mchezaji atambua umuhimu wa mechi hii na vile ambavyo tumeambiana kwa hali ilivyo ndani ya kambi na morali iliyopo imani yetu ya kupata pointi huku ni kubwa kuliko jambo jingine lolote.

“Hata katika mechi iliyopita na USGN tulihamasishana na wachezaji wenzangu na kweli wakaenda kupambana tena kutokea nyuma na tukapata pointi ya kwanza ugenini kwahiyo hata huku inawezekana. Tunaomba mashabiki waendelee kutuombea ikiwemo kuwa na imani kubwa na sisi kwani tunaelewa kile ambacho wanahitaji kutoka kwetu katika kila mechi iliyokuwa mbele yetu,” alisema Chama.

Simba inashuka uwanjani leo saa 4:00 usiku kwenye Uwanja wa Manispaa ya Berkane, mjini Berkane katika mechi yao ya tatu ya Kundi D ya michuano hiyo, ambalo Simba ni kinara.