UNAKUMBUKA dirisha dogo la usajili ambalo lilifungwa rasmi Januari 15, mwaka huu. Majina kama Chiko Ushindi na Clatous Chama yaliimbwa kweli.
Baada ya tambo za usajili kumalizika kwa sasa tayari idadi kubwa ya majembe hayo mapya yameanza kupiga kazi katika vituo vyao vipya vya kazi, ambapo wapo walioanza kuuwasha moto huku wengine wakiwa wanaendelea kusubiri muda wa kupata nafasi ya kuonyesha walivyonavyo.
Hapa tunakuletea orodha ya mastaa 11 ambao wamekamilisha usajili wao kwenye dirisha dogo ambao wanaweza kuunda kikosi hatari kama ifuatavyo;
1.Aboutwalib Mshery
Yupo zake ndani ya Yanga kwa sasa aliibuka hapo akitokea Mtibwa Sugar ni kipa namba mbili akiwa amecheza mechi nne za ligi ndani ya Yanga na hajafungwa mchezo hata mmoja kipa namba moja ni Diarra Djigui pia jina lake limeorodheshwa kwa mastaa walioitwa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
2. David Kameta
Licha ya hapo awali kuwa kwenye nafasi kubwa ya kutua Namungo, mlinzi huyu wa kulia wa Simba alimalizana na Geita Gold kwa mkopo dakika za mwisho kabla ya kufungwa kwa usajili akitokea Biashara United alipokuwa akihudumu kwa Mkopo.
Uwezo wake mkubwa uliwafanya Simba waamini anaweza kuwa mbadala wa Kapombe, anaingia katika kikosi hiki kama mlinzi wa kulia kutokana na uzoefu mkubwa alionao ana nafasi kikosi cha kwanza cha Geita Gold.
3. Adeyum Saleh
Baada ya kuhudumu ndani ya kikosi cha Yanga kwa kipindi cha miaka miwili. Kutokana na changamoto ya namba, nyota huyu wa zamani wa JKT Tanzania katika dirisha hili dogo la usajili aliamua kujiunga na klabu ya Geita Gold ambapo tayari ameanza kuuwasha moto.
4. Juma Nyoso
Nahodha wa zamani wa Barcelona ya bongo Klabu ya Ruvu Shooting na kitasa Mwandamizi, Juma Nyosso katika dirisha hili la usajili alijiunga na Geita Gold kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye safu ya ulinzi ya klabu hiyo kupitia uzoefu mkubwa alionao. Naye tayari ameanza kuwasha moto wake ndani ya Geita Gold.
5. Kelvin Yondani
Kama ilivyo kwa mkongwe mwenzake Nyosso, Yondani naye baada ya kuhudumu kwa msimu mzima ndani ya timu ya Polisi Tanzania ambapo alikuwa akihudumu kama nahodha, kwenye dirisha hili dogo la usajili aliamua kubadilisha mazingira na kumwaga wino ndani ya kikosi cha Geita Gold. Hakuna asiyejua uwezo wake na tayari ameanza kazi.
6. Salum Aboubakar ‘Sure Boy’
Amejiunga na Yanga akitokea ndani ya kikosi cha Azam ambapo alihudumu tangu mwaka 2007. Sure Boy ambaye ana uwezo wa kucheza nafasi zaidi ya moja uwanjani kwenye kikosi hiki atatumika kama kiungo mkabaji nafasi ambayo anaimudu vyema.
Uwezo aliouonyesha kwenye michuano ya kombe la Mapinduzi ni miongoni mwa vitu vinavyompa nafasi ya moja kwa moja kwenye kikosi hiki.
7. Crispin Ngushi
Winga mshambuliaji mpya wa Yanga kutokea ndani ya kikosi cha Mbeya Kwanza ambayo aliifungia mabao matatu msimu huu kabla hajajiunga na Yanga.
Amekuwa na wastani wa kufanya vizuri akiwa na Yanga ambapo kwenye mchezo wa kirafiki wa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mbuni FC ya Arusha alihusika kwenye penalti iliyozaa bao moja bado kwenye ligi amekuwa nje kwa muda kutokana na kutokuwa fiti.
8. Ibrahim Ajibu
Anajulikana kwa majina mengi ya utani kutokana na uwezo mkubwa alionao, ambao unafanya baadhi ya watu waamini ndiye mchezaji mzawa mwenye kipaji kikubwa cha soka kwa sasa licha ya mafanikio hafifu aliyonayo.
Amejiunga na Azam akitokea Simba ambako alikosa nafasi ya kucheza kwa misimu miwili aliyokuwepo hapo. Tangu ajiunge na Azam ameongeza kitu na anaonekana kuimarika zaidi.
9. Shaban Idd Chilunda
Amerejea tena ndani ya Azam akitokea nchini Morocco ambapo alikuwa akikipiga na klabu ya, Moghreb Athlétic de Tétouan. Chilunda amerejea ndani Azam kama mchezaji huru baada ya mkataba wake huko Morocco kumalizika.
Kutokana na uwezo wake mkubwa, Chilunda kwenye kikosi hiki anaweza kuhudumu nafasi ya mshambuliaji wa Kati.
10. Clatous Chama
Usajili ambao haukukauka midomoni mwa mashabiki na wadau wa soka hapa nchini, huku ukishereheshwa na taarifa za ‘majayanti’ wa soka Simba na Yanga kumalizana nae lakini mwishoni Simba walifanikiwa kutangaza rasmi kumrejesha.
Aliondoka na kujiunga na wababe wa Morocco klabu ya AS Berkane akiwa kaacha rekodi kali ya mabao nane na asisti 15, hivyo wengi wanasubiri kuona nini amerejea nacho.Ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu Pablo Franco.
11. Chiko Ushindi
Amejiunga na Yanga akitokea ndani ya kikosi cha TP Mazembe ya DR Congo ambapo kwenye mchezo wake wa kwanza tu pale Yanga walipovaana na Mbuni FC, alionyesha uwezo mkubwa ikiwemo kuhusika kwenye bao moja katika ushindi wa mabao 2-0. Kutokuwa fiti kulimuweka nje kwa muda.