Home Habari za michezo BAADA YA KUKIANGALIA KIKOSI CHA SIMBA KINAVYOCHEZA..CHUJI AMEGUNA ..KISHA AKASEMA HAYA…

BAADA YA KUKIANGALIA KIKOSI CHA SIMBA KINAVYOCHEZA..CHUJI AMEGUNA ..KISHA AKASEMA HAYA…


Kiungo fundi wa zamani wa kimataifa nchini, Athuman Idd ‘Chuji’ amekiangalia kikosi cha Simba, kisha akaamua kuwapa ujanja nyota wa timu hiyo Meddie Kegere, Pape Ousmane Sakho na wengine ili kuvuka hadi robo fainali ya michuano ya CAF.

Simba iliyopo Kundi D ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, inatarajiwa kuvaana na USGN ya Niger katika mechi ya mwisho ya kuamua hatma ya kutinga robo fainali baada ya wikiendi iliyopita kupoteza nafasi hiyo ikiwa ugenini.

Simba ilifungwa mabao 3-0 na Asec Mimosas ya Ivory Coast katika mechi iliyopigwa Benin na kuinyima fursa ya kuandika rekodi mpya ya kufuzu hatua hiyo ikiwa ugenini kwa timu za Tanzania tangu michuano ilipobadilishwa mwaka 2004.

Hata hivyo, Chuji aliyewahi kukipiga Simba, Yanga, Coastal Union, Singida United, Polisi Dodoma na Taifa Stars alisema kina Kagere na wenzake wana nafasi ya kufanya mambo katika mechi ya Aprili 3 kwa kutumia kila nafasi watakayoipata.

Chuji alisema kila mchezaji wa Simba anatakiwa kuzitumia kwa usahihi nafasi watakazopata bila ya kusahau kujilinda na kumsikiliza kwa umakini Kocha Pablo Franco ili kutimiza kiu ya mashabiki ya kuona Simba ikifuzu hatua inayofuata.

“Wanatakiwa kutuliza akili na wajue kipi cha kufanya hasa washambuliaji wenye kazi ya kufunga mabao, wasahau matokeo ya ugenini na kumaliza kazi Kwa Mkapa, naiona nafasi yao ya kusonga mbele kama watakuwa makini,” alisema Chuji.

Chuji aliyesifika enzi zake akicheza kwa kupiga mashuti makali na kuwa fundi wa pasi zenye macho, aliwaombea Simba ili wapate matokeo mzuri kwa nia ya kuipaisha klabu hiyo na Tanzania kwa ujumla kimataifa.

Katika Kundi D, Simba ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi saba sawa na ilizonazo RS Berkane ya Morocco, huku Asec ikiwa kileleni na alama 9 wakati USGN inashika mkia na alama zao tano, zote zina nafasi ya kusonga mbele.

SOMA NA HII  WAAMUZI HAWA WAWEKA REKODI MBELE YA RAIS MAGUFULI