Home Habari za michezo BAADA YA MIAKA MINGI KUPITA..KOTEI AFICHUA KILICHOMUONDOA SIMBA…AMTAJA HERSI WA YANGA…

BAADA YA MIAKA MINGI KUPITA..KOTEI AFICHUA KILICHOMUONDOA SIMBA…AMTAJA HERSI WA YANGA…


SIMBA ina viungo mafundi, lakini bado baadhi ya mashabiki wanaendelea kumuota James Kotei.

Mghana huyo alijitengenezea ufalme Msimbazi katika misimu mitatu akiupiga mwingi na kuisaidia timu hiyo kung’ara ndani na kimataifa kabla ya kutimka Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini Januari, mwaka juzi.

Licha ya uhakika wa kucheza, mkataba wake ulivyomalizika aliondoka nchini na kwenda Afrika Kusini, na baadaye akawa anatajwa kuhitajika na Yanga.

Katika makala haya Kotei anafichua dili zima lilivyokuwa na lilivyokufa na kufichua kwa sasa licha ya kuwa DTB iliyopo Ligi ya Championship, bado ameacha milango wazi kwa klabu za Simba, Yanga na Azam kumfuata. Mbali na kuzungumzia dili lake la Yanga, pia anafichua mipango aliyonayo DTB akipambana pamoja na wenzake kuipandisha Ligi Kuu Bara kwa lengo la kuongeza ushindani katika ligi hiyo iliyoasisiwa 1965. Endelea naye…!

KILICHOMUONDOA SIMBA

Mashabiki wa Simba walipigwa na butwaa kusikia Kotei anaondoka Msimbazi kwenda Afrika Kusini, lakini kiungo huyo anafichua kilichotokea kwa kusema baada ya mkataba kumalizika akiwa na Simba hakupokea ofa yoyote kwa mabosi wa timu hiyo na hata alipoamua kwenda nyumbani kwao hakupata chochote.

“Sikuona haja ya kusalia nchini, kwani ilionekana wazi sikuhitajika. Sikupata ofa ya kuongeza mkataba, hivyo nikaona ni vyema nitimke kwenda nyumbani ambako pia sikupata timu kwa haraka,” anasema.

Akiwa Ghana alipokea Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini na hakuona tabu kujiunga nayo.

“Sikuwa na ofa kutoka Simba. Pia Kaizer walipoonyesha nia ya kunihitaji, niliona ni sawa nitoke, lakini baada ya kwenda kule nilikutana na changamoto nyingi,” anasema.

“Nikiwa pale kocha alikuwa anataka amlete mchezaji wake, lakini Kaizer hawataki kocha alete mchezaji, hivyo alichokifanya ni kuniweka kwenye wakati mgumu kutaka nichague kuondoka kwa kutonipa muda wa kucheza.”

Kotei anasema alikosa nafasi ya kucheza na viongozi wa timu hiyo walisema hawawezi kumuingilia kocha upande wa kikosi.

“Nilienda Kaizer wakiwa wanafanya vizuri, hivyo waliweka wazi hawataki kumuingilia kwenye upangaji wa kikosi, bali walimuambia kama hanitumii basi waniachie niondoke na ndiyo tukakubaliana hivyo,” anasema.

AENDA ULAYA, APATA MAJANGA

Kotei anasema alilazimika kwenda kucheza soka la timu ndogo Ulaya katika timu ya Slavia iliyopo Belarus baada ya kukaa nje ya uwanja muda mrefu. Licha ya kwenda bado alijikuta katika wakati mgumu kutokana na kupata majeraha yaliyomfanya acheze miezi sita.

“Nilipata (jeraha la la) enka, lakini ujue wale jamaa hawana kawaida ya kumzingatia mchezaji ambaye amepata majeraha, kwa hiyo nikaamua mwenyewe kuondoka baada ya kutopata stahiki zangu,” anasema.

ISHU YA KUTUA YANGA

Kotei anasema wakati anaondoka Kaizer Chiefs kwenda Slavia alipokea ofa ya Yanga, lakini moyo wake ulikuwa unasita akiona kama anaweza kuisaliti Simba kwa namna ambavyo alikuwa ameishi nayo nchini na akiamini anaweza kurejea tena.

Anasema akiwa Beralus alipokea tena ofa ya Yanga na hapo Simba haikumfuata, ndipo akaona ni wakati sahihi kwake kujiunga na wana Jangwani.

Anasema alikuwa na kila sababu ya kutua Jangwani, lakini alishangaa kuona hali ya ukimya, licha ya kukubaliana kila kitu na uongozi wa klabu hiyo na alikuwa anasubiri tiketi ya ndege atue Dar.

“Walipokuja Yanga mara ya pili baada ya Simba kutokuja nilisema acha nije, lakini kilitokea kitu kama siasa kwamba nilishacheza Simba ndio maana hawakurudi tena. Kifupi ni kwamba wao ndio waliokwamisha dili,” anasema.

“Napofanya kazi, mapenzi yangu huwa hapo hata kama nilikuwa sehemu fulani muda wa nyuma. Kwa hiyo hilo dili lilishindikana lakini linaweza kuwepo.”

SOMA NA HII  'MPAPATUKO' WA NBC PREMIER LEAGUE KUENDELEA TENA LEO...RATIBA NZIMA IKO HAPA....

AVUTWA DTB, AUKUBALI MZIKI

Kotei anasema baada ya kuondoka Slavia alijiunga na Sohar FC, lakini hakukaa sana na baada ya hapo alipokea ofa ya timu ya DTB.

Kiungo huyu mkata umeme anasema baada ya kupokea ofa hiyo aliifuatilia namna ilivyo na majina makubwa ya wachezaji yaliyopo yalimvutia. “Niliangalia nikaona kuna wachezaji wakubwa kama Amissi Tambwe, Tafadzwa Kutinyu na Nicholas Gyan nikasema hii timu ina mipango mizuri, kwa hiyo nina kila sababu ya kuja hata kama haipo Ligi Kuu,” anasema.

“Hata nilivyoongea na mke wangu aliniambia hauwezi kujua Mungu amekupangia nini, kwa hiyo nije Tanzania ni kama nyumbani inawezekana ikatokea safari nyingine nikiwa hapa.”

Kotei anasema akiwa DTB msimu huu kwenye Ligi ya Championship amekutana na ugumu mkubwa wa ligi kutokana na kila timu kupambana kupanda Ligi Kuu.

“Ujue hapa ndio sehemu ambayo inakufanya uende Ligi Kuu, kwa hiyo ni pagumu kwa sababu kila mmoja anawaza namna ya kusogea juu, ni hatari, lakini tunapambana,” anasema Kotei.

KAMBI KOKOTE

Kotei anaweka wazi lengo lake la kwanza ni kuhakikisha DTB inapanda Ligi Kuu na baada ya hapo kama atapokea ofa kutoka Yanga, Simba, Azam au timu yoyote anaweza kuondoka.

Anasema jambo la kwanza atawasikiliza mabosi wake wa sasa baada ya hapo ndio anaweza kufanya uamuzi kwa sababu hapendi kufanya kitu cha kuumiza mtu ambaye amemjali.

“Nikiwa sehemu napenda hata nikiondoka basi nitoke vizuri na sio kufanya usaliti. Nimepitia mambo mengi magumu sana tangu nitoke Simba, kwa hiyo siwezi kufanya kitu cha ajabu kwa mtu ambaye amenithamini.”

AMTAJA HERSI

Kama unadhani Kotei amepotezana moja kwa moja na Yanga unajidanganya, kwani mchezaji huyo anasema bado ana urafiki mkubwa na mjumbe wa Kamati ya Usajili, Hersi Said.

Kotei anasema ni rafiki i wa Hersi na ndiye alimfuata wakati Yanga wanamtaka na hata dili hilo lilipokimbia wanawasiliana.

“Hersi ni mtu safi na tunazungumza mpaka sasa. Huwa tunasalimiana na kujuliana hali mara kwa mara na hata dili langu lilipokwama aliniambia alikuwa anataka kunirejesha Tanzania.

“Hii ni kazi yangu na mimi sina mapenzi na timu, bali nafanya kazi kwa hiyo hata ikitokea wanakuja kwa mara nyingine wawe na imani kubwa kwangu,” anasema Kotei.

YACOUBA YANGA

Kotei anasema baada ya yeye kushindwa kutua Yanga alihusika katika dili la mshambuliaji Yacouba Sogne kujiunga na timu hiyo msimu uliopita.

Kiungo huyo anasema aliulizwa na Hersi kama Yacouba anaweza kucheza Yanga na yeye aliwaambia ni mchezaji mzuri na atawasaidia kwa sababu anamfahamu na alichofanya alimuambia wakala wao Yacouba anahitajika.

“Nilikuwa namfahamu toka Asante Kotoko na niliwaambia kabisa ataweza kuwasaidia kwa sababu ni mchezaji mpambanaji na anaweza kufiti kwenye ligi hii,” anasema Kotei.

“Hivyo Injinia (Hersi) nilimwambia ukweli atawafaa. Kwa wachezaji ambao nilikuwa nao Ghana ukiniuliza nitakuambia huyu anaweza kucheza Tanzania huyu hawezi kwa sababu ligi ya Tanzania ina ugumu wake, kama isingekuwa majeraha angeendelea kufanya vizuri.”

AMKUBALI MKUDE

Kotei anasema Jonas Mkude ni mchezaji ambaye ana uzoefu mkubwa Simba na ni jambo zuri kumuona akiendelea kucheza.

Anasema: ”Mimi na Mzamiru (Yassin) tulikuwa tunacheza kwenye eneo la kukaba sana halafu yeye (Mkude) tulikuwa tunamuacha kama namba nane awe huru kucheza.”

Credit :- MwanaSpoti