Home Habari za michezo ENDAPO WATAFUZU ROBO FAINALI…KWA VYOVYOTE SIMBA WAOMBE WASIPANGWE NA HAWA CAF…

ENDAPO WATAFUZU ROBO FAINALI…KWA VYOVYOTE SIMBA WAOMBE WASIPANGWE NA HAWA CAF…


HABARI ndio hiyo. Simba ina dakika 90 tu za kuamua hatma yake katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na Jumapili ijayo itaikaribisha US Gendarmarie ya Niger katika pambano la kukamilisha ratiba ya mechi za Kundi D.

Mechi hiyo ndiyo itakayoamua kama Simba iende robo fainali na kuandika rekodi mpya kwa klabu za Tanzania katika michuano hiyo au iage.

Wakati mastaa wa timu hiyo wakiingia kambini leo kuanza maandalizi ya mchezo huo wa mwisho utakaochezwa Aprili 3 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, hesabu kwa Simba ikitoboa hapo na kutinga robo fainali zitakuwa ni kali zaidi ya sasa.

Moto utawaka zaidi katika hatua hiyo kutokana na uwezekano wa kukutana na timu zitakazofuzu hatua hiyo kutoka makundi mengine matatu ya michuano hiyo.

Kwa namna yoyote ile Simba haitoweza kumaliza nafasi ya kwanza kwenye kundi lake hata kama itashinda dhidi ya USGN.

Iko hivi, matokeo ya aina yoyote katika mchezo kati ya RS Berkane na Asec Mimosas mojawapo itaongoza kundi D na Simba ikiifunga Gendarmerie itafikisha pointi 10 na itamaliza ya pili.

Kama RS Berkane itaifunga Asec itamaliza juu ya Simba, japo itakuwa na pointi sawa kwani watabebwa na kanuni ya kupata matokeo mazuri dhidi ya Simba katika mechi zao mbili na ndio cha kwanza kutazamwa kikanuni iwapo timu mbili zitalingana pointi.

Lakini kama Asec itapata ushindi, itafikisha pointi 12 ambazo haziwezi kufikiwa na Simba na ikiwa mechi yao itamalizika kwa sare, itafikisha pointi 10 sawa na Simba lakini nayo itabebwa na kanuni ya kuwa na matokeo bora dhidi ya Simba ukizingatia wao walifungwa 3-1 hapa Dar es Salaam na wakashinda 3-0 nyumbani huko Benin.

Hata hivyo, ikiwa Simba itamaliza ya pili, inaweza kuwa nafuu zaidi kwao kuliko kumaliza nafasi ya kwanza kutokana na ubora, ukubwa na uzoefu wa timu ambazo huenda ingekutana nazo robo fainali.

Kwa namna msimamo wa makundi manne ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu yalivyo, timu zitakazomaliza nafasi ya pili nyingi zinaonekana zitakuwa tishio kwa Simba.

Upo uwezekano mkubwa timu zinazofanya vizuri katika michuano ya klabu Afrika, zilizo na uwekezaji mkubwa wa kifedha pamoja na uzoefu wa kutosha zikamaliza nafasi ya pili na kwa mujibu wa kanuni za michuano hiyo zitakutana na zitakazomaliza nafasi ya kwanza.

SOMA NA HII  HAWA HAPA MASTAA 5 WA YANGA WATAKAOKOSEKANA LEO..KAZE ASHINDWA KUJIZUIA...AFUNGUKA...

Simba kama itamaliza nafasi ya pili, itakutana na kinara wa kundi A (Al Ahli Tripoli ya Libya) ambayo mafanikio makubwa ni kutinga nusu fainali ya Kombe la Washindi Afrika mwaka 1984 ingawa imezidiwa na Simba kimafanikio.

Timu hatari zaidi kwa Simba ni Pyramids FC ya Misri iliyofanya usajili mkubwa wa wachezaji.

Lakini mbali na kushinda mechi yake ya mwisho dhidi ya US Gendarmerie, Simba itapaswa kuombea Al Ahli Tripoli ipate ushindi katika mechi ya mwisho ya kundi lake ugenini dhidi ya CS Sfaxien ama itoke sare.

Katika kundi B, kinara hadi sasa ni Orlando Pirates yenye pointi 12 ikifuatiwa na Al Ittihad ya Libya yenye pointi 10 na zitakutana zenyewe katika mechi zao za mwisho.

Al Ittihad ndio timu inayoonekana sio mfupa mgumu zaidi kwa Simba kati ya zilizo nafasi ya pili kwenye makundi kwa sasa huku nafasi ya kwanza ikiwa chini ya Orlando Pirates iliyowahi kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika 1995, kufika fainali ya michuano hiyo mwaka 2013 huku ikitwaa taji la Super Cup 2016.

Katika kundi C, TP Mazembe inayoshika nafasi ya pili ndio inaonekana kuwa tishio zaidi kwa Simba kulinganisha na Al Masry inayoongoza msimamo wa kundi hilo. Mafanikio makubwa kwa Al Masry inayoongoza kundi C la Mazembe, ni kufika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2002 na mwaka 2018.

Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally alisema kwa sasa wanawazia kwanza mechi yao ya mwisho dhidi ya US Gendarmerie.

“Kwa sasa mipango na mikakati yetu ni kupata ushindi katika mechi yetu ya mwisho dhidi ya Gendarmerie na baada ya hapo ndio mipango ya robo fainali itaanza.”

“Tunatakiwa kufuzu kwanza kisha tutaona tutapangiwa na nani lakini sisi Simba tuko tayari kukabiliana na timu yoyote,” alisema Ally.

Naye beki wa zamani wa Simba, Boniface Pawasa alisema Simba inayo nafasi ya kufika mbali katika mashindano hayo ingawa inapaswa kuhakikisha inafanyia kazi udhaifu wake.

“Simba iko vizuri na inaweza kupambana na timu yoyote Afrika na ikafanya vizuri lakini kuna maeneo inapaswa kuyashughulikia kama kuimarisha safu ya ulinzi na washambuliaji wake kuhakikisha wanatumia nafasi za mabao,” alisema Pawasa.