Home Makala KUHUSU ISHU YA UJENZI WA UWANJA WA SIMBA ULIOANZIA TWITTER…KUMBE NI SIASA...

KUHUSU ISHU YA UJENZI WA UWANJA WA SIMBA ULIOANZIA TWITTER…KUMBE NI SIASA TUPU…HAKUNA KITU..


Jumamosi moja yenye heka heka hivi ndani ya Jiji la Dar es Salaam. Ni Jumamosi ya Desemba 11 mwaka jana. Ilikuwa Jumamosi ya pambano la watani wa Jadi Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa. Ni siku yenye hisia tofauti.

Ni Jumamosi hii Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alionekana zaidi kwenye Mtandao wa Instagram kuliko sehemu nyingine yoyote.

Haikuwa siku nzuri sana kwake. Ya kumkuta yalimkuta pale kwa Mkapa na akaishia kulitazama pambano hilo kwenye televisheni.

Ni Jumamosi hii iliyozaa wazo la Simba kuwa na Uwanja wake wa mashindano. Baada ya Barbara kuzuiwa kuingia na watoto wadogo kwenye Ukumbi wa VVIP pale kwa Mkapa, ndipo Simba ikafikiria kujenga uwanja wake wa mashindano. Ni ajabu na kweli.

Timu yenye miaka zaidi ya 80 inafikiria kujenga uwanja wa mashindano kwa sababu mtendaji wake alizuiwa kuingia na watoto wadogo katika sehemu wanayokaa Wageni wa heshima. Tanzania haiishi vituko. Lakini unadhani hili ni tatizo kubwa? Hapana, subiri nitakueleza tatizo zaidi liko wapi.

Tatizo ni namna jambo lenyewe la Uwanja lilivyoanza. Ujenzi ukaanzia huko Twitter. Mtendaji Mkuu wa zamani wa timu hiyo, Crecentus Magori akasema kitendo cha Barbara kunyanyaswa kabla ya pambano hilo la watani kiwe msukumo wa kujenga uwanja wao.

Wazo hilo likatiliwa mkazo na Mwekezaji wa timu hiyo, Mohammed Dewji ‘MO’.

Naye akaitumia Twitter hiyo hiyo kusema kwamba muda wa Simba kuwa na uwanja wake umefika na yeye atachangia Sh2 bilioni. Ikaonekana kama habari njema kwa Wanasimba wote.

Lakini hiki ndio kilikuwa pengine ndio kituko kikubwa zaidi. Kabla ya kufahamu gharama za uwanja wenyewe, mwekezaji ametangaza kutoa Sh2 bilioni.

Ni kiasi kidogo sana kwenye ujenzi wa Uwanja. Nadhani mwekezaji alipaswa kusubiri kwanza tathmini ifanyike.

Uwanja wa Benjamin Mkapa ulijengwa Zaidi ya miaka 15 iliyopita. Uligharimu zaidi ya Sh56 bilioni. Wiki hii huko Senegal wamezindua uwanja wao wa kisasa unaoingiza mashabiki 50,000 ambao umegharimu zaidi ya Sh500 bilioni. Leo hii MO anatangaza kuchangia Sh2 bilioni kwenye Ujenzi wa Uwanja wa Simba. Kuna uwanja hapo? Akili mtu wangu.

SOMA NA HII  SASA NI KAZI YA USAJILI, KAZI IACHWE MIKONONI MWA KOCHA

Vituko havikuishia hapo. Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara akaita Waandishi wa Habari kwenye ofisi zao Masaki.

Akatangaza kuanza kwa mchakato wa ujenzi wa uwanja huo. Mchakato ukaanza kwa kuhamasisha Wanasimba wote kuchangia.

Zikawekwa namba za mitandao ya Simu za kuchangia. Zikawekwa akaunti za benki. Mchakato ukaanza. Nini kimetokea baada ya hapo?

Ni miezi miwili sasa tangu kufunguliwa kwa mchakato huo. Kwanza hadi leo, Simba haijasema inataka kukusanya kiasi gani cha fedha kwa ajili ya ujenzi huo. Haijasema uwanja huo utatengenezwa wapi. Haijatoa ramani ya uwanja. Yaani ni siasa tupu.

Ajabu zaidi ni tangu mchakato wa kuchangisha ufunguliwe, mpaka leo Simba haijawahi kusema imekusanya kiasi gani cha fedha. Yaani watu wanachanga tu kwa miezi miwili na hakuna anayejua kimepatikana kiasi gani. Inashangaza sana.

Yawezekana hii ndio harambee ya ovyo zaidi kuwahi kufanyika duniani. Hakuna hamasa ya kuchangia. Hakuna taarifa za michango. Watu hawafahamu wanatakiwa wachange kiasi gani. Uwanja wanaochangia hawajui utajengwa lini na wapi.

Hii ndio sababu nasema mchakato huo umekaa kisiasa. Ni zoezi lililokaa kimihemko Zaidi. Ina maana kama Barbara angeruhusiwa kuingia na watoto hao wadogo pale kwa Mkapa, basi mpaka leo Simba isingekuwa na mpango huo. Yaani kwa kifupi ni kwamba Simba haijawahi kuwa na mpango wa kujenga uwanja wake.

Hii mi mihemko tu iliyoanzia pale kwa mkapa, ikahamia Instagram na kisha Twitter. Mengine yote ni siasa.

Kwa kifupi sioni Simba ikiwa na uwanja wake leo ama kesho. Sioni mchakato huu ukipiga hatua yoyote.

Ni kupotezeana tu muda. Ni afadhali Yanga hawana mpango wa uwanja. Kila siku wanazindua nyimbo mpya ya kusifia klabu yao na watendaji wake.

Makala haya yaliandikwa kwanza kwenye wavuti la Mwanaspoti