Home Habari za michezo BENCHIKA KUENDELEZA REKODI LEO MBELE YA ASEC MIMOSAS?….KRAMO AWAPA TAHADHARI…

BENCHIKA KUENDELEZA REKODI LEO MBELE YA ASEC MIMOSAS?….KRAMO AWAPA TAHADHARI…

Habari za Simba leo

Kikosi cha Simba tayari kipo Ivory Coast kwa mechi ya Kundi B ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya wenyeji, Asec Mimosas, huku ikipata jeuri kutokana na rekodi tamu za kocha mkuu Abdelhak Benchikha kwa mechi za CAF na hasa dhidi ya WaIvory Coast hao wanaoongoza kundi.

Simba iliondoka Dar es Salaam juzi ikiwa na wachezaji 21, ikiwaacha nyumbani kipa Ayoub Lakred na mshambuliaji mwenye mabao mengi kwa timu hiyo kwenye michuano hiyo, Willy Onana aliyefunga mawili .

Licha ya mechi hiyo kuangaliwa kama ni vita kali kwa Simba mbele ya Asec ambayo haijawahi kupoteza nyumbani mbele ya Simba, lakini rekodi tamu alizonazo Benchikha katika ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika akiwa na uzoefu wa miaka zaidi ya 20 zinakipa jeuri kikosi hicho kilichopo nafasi ya pili.

Benchikha ameandika rekodi akiwa na timu tofauti, ikiwemo kutwaa taji la Shirikisho msimu uliopita alipoifunga Yanga katika fainali akiwa na USM Alger kisha kubeba CAF Super Cup kwa kuwachapa wababe wa Afrika, Al Ahly ya Misri kabla ya kujiuzulu na baadaye kuibukia Simba.

Uzoefu huo ni miongoni mwa sifa zilizoishawishi Simba kuvunja benki na kumdondosha Msimbazi kumpatia chama lenye mastaa wapambanaji kama Kibu Denis, Sadio Kanoute na Che Malone Fondoh na mafundi kama Clatous Chama, Mohamed Hussein na Willy Onana pamoja na wafia timu kama John Bocco, Shomari Kapombe na Henock Inonga na wengine kibao.

Hata hivyo, Benchikha, tangu ametua Simba ameonyesha kimataifa sio mnyonge kwani licha ya kuikuta timu hiyo ikiwa katika kiwango kibovu, lakini aliiongoza kwenye mechi tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika na kuvuna pointi nne kibabe.

Mkali huyo alianza kuiongoza dhidi ya Jwaneng Galaxy ugenini Botswana na kutoka suluhu, kisha akaenda Morocco kwa Wydad wakafungwa jioni bao 1-0 kabla ya kulipa kisasi mabao 2-0 katika mechi ya marudiano Desemba 19, 2023 Kwa Mkapa – yote yakiwekwa kambani na Onana ambaye hayupo Abidjan kwa sasa.

Baada ya takriban miezi miwili kupita, sasa Benchikha na Simba wanarejea katika mechi za kimataifa kwa kuivaa Asec iliyowatoa mastaa kibao akiwemo Pacome Zouzoua, Stephane Aziz Ki na Kouassi Attohoula Yao wa Yanga sambamba na Kramo Aubin wa Simba.

Utamu ni kwamba, Benchikha anaijua vyema Asec, kwani haijawahi kufunga hata bao moja dhidi ya timu alizozinoa kwani msimu uliopita alikutana nayo mara mbili akiwa na USM Alger na kuchukua pointi katika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho.

Mechi ya kwanza ilipigwa Ivory Coast, USM Alger ikatoka suluhu, kisha kwenda kushinda 2-0 nyumbani na kutinga fainali kukutana na Yanga ambapo ilifaidia na kanuni ya bao la ugenini baada ya matokeo ya mwisho kuwa sare ya 2-2, Yanga ikifungwa nyumbani 2-1 na kushinda ugenini bao 1-0, hivyo taji kubebwa na USM Alger.

Kwa hesabu hizo ni wazi kama Benchikha akiendelea na rekodi huenda leo akaivusha Simba kwenda robo fainali iwapo itashinda mechi hiyo.

Simba iko kundi B, nafasi ya pili na alama tano baada ya mechi nne chini ya Asec wenye pointi 10, huku Jwaneng ikiwa ya tatu na alama nne na Wydad ikiburuza mkia na alama tatu.

Ili Mnyama avuke kuendeleza rekodi ya kucheza robo, inahitaji kushinda mechi mbili zilizosalia ikiwamo ya mwisho dhidi ya Jwaneng kwani itafikisha pointi 11. Mechi na Jwaneng itachezwa Machi 2 kwenye Uwanja wa Mkapa.

Benchikha anajiamini na amewaeleza wachezaji wake kuwa, “ili uwe mkubwa unatakiwa kushindana na wakubwa na kushinda. Ni nafasi ya Simba kuonyesha ukubwa na pia nafasi ya mchezaji mmoja mmoja kufanya jambo kwa ukubwa. Hatuko kwenye eneo baya, lakini pia hatuko salama. Ushindi ni lazima kwenye mechi mbili zijazo na naamini kwa mipango tuliyoweka tutaenda kushinda na kuvuka hatua hii.”

Mratibu wa timu hiyo, Ally Abbas alisema timu ilifika salama na Katika mechi tano za awali zikiwamo tatu za Ligi ya Mabingwa na mbili za Kombe la Shirikisho, kila timu imeshinda nyumbani mara mbili na mchezo mmoja ukaishia kwa sare.

Katika hatua nyingine, Aubin Kramo, mchezaji wa Simba aliyesajiliwa mwanzoni mwa msimu huu akitokea Asec Mimosas, ametoa ramani ya ushindi Msimbazi.

Kramo hajacheza kutokana na kuandamwa na majeraha jambo lililowafanya vigogo wa Msimbazi kumuondoa kwenye usajili hadi msimu ujao huku wakimpa huduma na stahiki muhimu akiwa Dar es Salaam.

Simba imemuacha Kramo Bongo, lakini imeondoka na maoni yake namna ya kushinda mchezo huo kutokana na uzoefu wake akiwa Asec Mimosas kwani alikulia kwenye akademi ya timu hiyo kabla ya kwenda kupata uzoefu FC San Pedro na African Sports na baadaye kurejea kikosini hapo na kufanya makubwa yaliyowashawishi viongozi wa Simba kumsajili.

Kramo amesema Asec ya sasa ina wahezaji wengi vijana na wenye ndoto za kusonga mbele zaidi hivyo watacheza dhidi ya Simba kwa nguvu ili kuonekana na kuitaka Simba kuwa makini kutumia vyema pengo la mshambuliaji Sankara Karamoko aliyekuwa tegemeo kikosini hapo lakini mwezi Januari aliuzwa Wolfsberger AC ya Austria.

“Asec ni timu nzuri na ina wachezaji wenye uchu wa kufanya vizuri zaidi. Hilo linawapa nguvu ya kupambana kwa dakika 90 ili waisaidie na pia waonekane. Simba ina nafasi ya kushinda. Matumizi ya mapengo yaliyopo kwa Asec yanaweza kuisaidia Simba kushinda na kuongeza alama.”.

SOMA NA HII  KISA KUKOSA NAMBA KIKOSI CHA KWANZA YANGA...MAKAMBO ALIA NA UONGOZI...AKASIRIKA KUTOPANGWA...