Home news SAKHO – TULIENI..MIMI BADO SAANNA YANI…, BARBARA NA TRY AGAIN WACHORA RAMANI...

SAKHO – TULIENI..MIMI BADO SAANNA YANI…, BARBARA NA TRY AGAIN WACHORA RAMANI YA UBINGWA CAF…


LAZIMA kieleweke, Simba ya mwaka huu haitaki kuacha chochote. Yaani baada ya kutwaa Kombe la Mapinduzi kule Zanzibar, Wekundu wa Msimbazi wanalitaka taji la tano mfululizo la Ligi Kuu Bara, Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) na hadi kule CAF wana jambo lao.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema kiu ya mafanikio waliyonayo ni kubwa na wanaamini watatoboa kwenye mashindano yote kutokana na mipango sahihi waliyoweka.

Alisema nadhani kila mmoja ameona ambavyo Simba imecheza katika kiwango bora dhidi ya timu kubwa kama RS Berkane hicho kiwango si kama kimekuja tu bali ni maandalizi ya kutosha waliyopata wachezaji.

“Benchi la ufundi limefanya kazi ya kutosha kuandaa timu kimbinu na kiufundi zaidi, wachezaji wamekwenda kupambana vya kutosha na kuhakikisha tunashinda na imekuwa hivyo,” alisema Try Again na kuongeza;

“Hatuna wasiwasi ushirikiano unaotoka kwetu uongozi kwenda kwa wachezaji na benchi la ufundi Simba, tunaamini tutafanya vizuri zaidi katika mashindano haya na kufika hatua za mbele tofauti na misimu mingine yote katika mashindano.”

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alisema nafasi ya kufuzu hatua inayofuata ni kubwa kutokana na mipango waliyonayo na bahati nzuri wanahitaji pointi tatu katika michezo miwili.

Barbara alisema viongozi wanawapatia vitu vya msingi wachezaji na benchi la ufundi kila wanachohitaji tena kwa wakati ili kuwa na muendelezo mzuri na kufikia mafanikio siku zijazo.

“Viongozi na benchi la ufundi tutawasiliana na kuangalia maeneo yapi yenye upungufu tuboreshe zaidi ili kufanya vizuri michezo inayofuata,” alisema na kuongeza;

“Kulingana na viongozi ambavyo tumejipanga na malengo ya timu yalivyo ninaamini hatushindwi.”

SAKHO AFUNGUKA

Mfungaji wa bao lililoiweka Simba kileleni mwa msimamo wa Kundi D dhidi ya Berkane ya Morocco juzi, Pape Ousmane Sakho ametaja siri ya makali yake ya siku za karibuni akisema ni kujiongeza dozi ya mazoezi binafsi baada ya yale anayofanya na wenzake.

“Nimejisikia mwenye amani na furaha kufunga katika mechi iliyopita na natamani kuendelea kufanya hivi zaidi. Nafanya mazoezi yangu binafsi mengi zaidi sasa baada ya yale ya timu ili kuimarika na kufikia kile ninachotaka kufanya,” alisema na kuongeza.

SOMA NA HII  SIKU KADHAA BAADA YA YANGA KUZINDUA JEZI...SIMBA WAIBUKA NA KUTAMBA KUHUSU JEZI ZAO..WADAI ZINATOKA ULAYA...

“Kabla ya mechi kuna maelekezo huwa napokea kutoka kwa kocha (Pablo Franco), kwenda kuyafanya uwanjani. Baada ya mechi kumalizika alinieleza kuwa amefurahishwa kile nilichokifanya muda wote niliocheza.”

Alisema katika kila mechi anayocheza anatamani kufunga bao ili kuirahisishia timu yake kupata ushindi kama alivyofanya dhidi ya RS Berkane.

“Kulingana na majukumu ya nafasi yangu nikishindwa kufunga bao natamani kuwa msaada kwa mchezaji mwingine ili kutimiza malengo ya timu,” alisema Sakho na kuongeza;

“Napenda kutoa pasi ya mwisho, kuhusika kwenye kufunga bao, kuwasumbua mabeki wa timu pinzani ili wachezaji wengine wa Simba wawe na kazi rahisi.”

Sakho alisema mashabiki wa Simba wasiwe na wasiwasi kwani kulingana na malengo waliyojiwekea wachezaji timu yao ina kila sababu ya kusonga hatua za mbele zaidi.

Alisema wanataka kuweka rekodi katika mashindano hayo ikiwezekana kuchukua mpaka ubingwa ili kuonyesha kuwa Simba ni moja ya timu kubwa Afrika na hilo linawezekana.

Sakho alisema kuhusu kiwango chake kuzidi kuimarika kila siku kwenye michezo ya ndani na kimataifa ni kupenda kujituma muda wote anapokuwa katika majukumu kwenye mazoezi na mechi.

“Bado sijafikia katika kile kiwango changu ninachojifahamu kutokana na majeraha, kuna nyakati yalinirudisha nyuma ila naamini nitakuwa bora zaidi ya hapo na kuupigania Simba ikiwemo kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara,” alisema Sakho.

Winga Pater Banda alisema kufanya vizuri katika mechi hiyo na RS Berkane ni chachu kwao kufanya hivyo katika mechi inayofuata ili kufuzu hatua ya robo fainali.

“Kila mchezaji aliyepata nafasi ya kucheza alijitolea kwa kiasi kikubwa ndio maana tumefanikisha malengo yetu ya kushinda nyumbani,” alisema Banda.

Kiungo Clatous Chama aliwapongeza wachezaji wenzake wote waliopigana mpaka dakika ya mwisho kuhakikisha Simba inapata ushindi na iwe hivyo katika michezo miwili iliyobaki.