Home news WAKATI WATU WAKIANZA KUMUELEWA…BANDA KAWATAZAMA WEE..KISHA AKASEMA HAYA…PABLO KAKOLEZA CHUMVI..

WAKATI WATU WAKIANZA KUMUELEWA…BANDA KAWATAZAMA WEE..KISHA AKASEMA HAYA…PABLO KAKOLEZA CHUMVI..


WINGA kutoka Malawi, Peter Banda (21), ameanza kuonyesha makali yake ndani ya kikosi cha Simba, ikiwamo kufunga na kuasisti, lakini mwenyewe amesema bado hajaridhika na kiwango alichokionyesha na sasa anajipanga zaidi ili kuwaonyesha watu uwezo alionao na kuisaidia timu hiyo.

Banda alisajiliwa na Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea Sheriff Tiraspol ya Moldova, alikokuwa akicheza kwa mkopo kutokea Big Bullet ya kwao Malawi, hata hivyo alikuwa na mwanzo mbaya, lakini tangu arejee kutoka Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2021 zilizofanyika Camareoon akiwa na Malawi, ameonekana moto, ikiwamo Jumatatu kutoa asisti tamu ya krosi iliyozamishwa wavuni kwa kicha na Meddie Kagere na kuipa Simba ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji.

Katika mechi za hivi karibuni kuanzia zile za kimataifa hadi za Ligi na Kombe la Shirikisho la Azam Sports, Banda ameonekana kumshawishi kocha Pablo Franco na kuwa miongoni mwa wachezaji wa Simba wenye uhakika kuanza katika kikosi cha kwanza mara kwa mara na hajamuangusha Mhispaniola huyo kwa kuwa msaada mkubwa kikosini, kwani katika mechi tano za mwisho amehusika katika mabao mawili kati ya tisa ya timu hiyo akifunga bao moja na kuasisti.

Hata hivyo, akizungumza juzi, Banda alisema, licha ya kazi nzuri aliyoifanya lakini bado hajafikia kiwango anachokitaka na anaendelea kupambana ili kuhakikisha anaisaidia Simba kufikia malengo pamoja na kuuonyesha umma ubora wake ikiwemo kuwaziba midomo wale waliombeza mwanzo.

“Ninachokihitaji kwa sasa ni kuwaonyesha watu ubora uliondani yangu katika kuisaidia timu kufikia malengo yake. Nashukuru benchi la ufundi kwa kuniamini na kunipa nafasi,” alisema Banda na kuongeza;

“Nitaendelea kupambana ili kurudisha hali yangu ya kujiamini itakayonifanya kuwa bora na kufurahia zaidi maisha yangu ndani ya Simba na naamini hilo litatimia kwani tuko pamoja na wachezaji wenzangu, wananisapoti kwa kila kitu hivyo mashabiki wa Simba waondoe shaka juu ya timu yao kwani tupo hapa kuwafurahisha zaidi na zaidi.”

Kocha Pablo alimuelezea Banda kuwa mchezaji mdogo mwenye uwezo mkubwa sana na kila sifa ya kuchezea timu kubwa kama Simba.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA SPOTI XTRA JUMAPILI

“Banda ni mchezaji mzuri na mwenye kipaji kikubwa, kila siku anaonesha kuimarika na naamini kwa kushirikiana wote tutafikia malengo,” alisema Pablo.

Banda amekuwa akianza kama winga wa kulia na kushoto anaanza Pape Sakho na wametengeneza maelewano na wenzao.