KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, ameweka wazi kuwa licha ya mwenendo bora walionao msimu huu, bado haridhishwi na kiwango cha umakini wa kutumia nafasi za kufunga kwa safu yake ya ushambuliaji iliyo chini ya Fiston Mayele.
Nabi alisema katika kutatua tatizo hilo, ni wazi wanapaswa kulifanyia kazi kwa juhudi kubwa kuiongezea makali safu hiyo ili kutimiza lengo la kuibuka mabingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.
Yanga wamekuwa na wakati mzuri msimu huu ambapo mpaka sasa wanaongoza msimamo wa ligi na pointi zao 51 walizokusanya katika michezo 19. Hivi sasa wanajiandaa na mchezo unaofuata wa ligi dhidi ya Simba utakaochezwa Aprili 30, mwaka huu.
Vinara hao wa Ligi Kuu Bara, Jumapili iliyopita walifanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports, mara baada ya kuwaondosha Geita Gold kwa penalti 7-6.
Kocha Nabi alisema: “Tumekuwa na wakati mzuri katika michezo mingi msimu huu, lakini mara kadhaa nimekuwa nikiongea kuhusu suala la changamoto ya kutumia nafasi nyingi ambazo tunazitengeneza.
“Mfano kwenye mchezo dhidi ya Azam na hata ule tuliocheza dhidi ya Geita Gold, tuliendelea kuwa na baadhi ya makosa hususani katika suala la kutumia nafasi na kufunga mabao, nadhani bado tuna kazi kubwa ya kufanya.
“Kadiri msimu unavyoelekea ukingoni na michezo inakuwa migumu, hivyo tunahitaji mabao kwa kila nafasi ili kupata matokeo mazuri yasiyokuwa na presha.”
Katika Ligi Kuu Bara msimu huu, Yanga imefunga mabao 33, ikiwa ndiyo timu yenye mabao mengi baada ya kucheza mechi 19. Inafuatiwa na Simba na Azam ambazo kila moja imefunga mabao 23.