BAADA ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Orlando Pirates kwenye mchezo wa kwanza wa robo fainal ya Kombe la Shirikisho Afrika, Simba SC wamesema wanakwenda Afrika Kusini kumalizia kazi.
Juzi Jumapili, Simba iliibuka na ushindi huo katika Uwanja wa Mkapa, Dar, Jumapili ijayo watarudiana nchini Afrika Kusini ambapo mshindi wa jumla atakwenda nusu fainali.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo wa juzi Jumapili, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema kwamba tayari wana uhakika wa kutinga ya nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kushinda nyumbani.
Ally aliongeza kwamba, kilichobaki sasa ni kuona wanakwenda kuzicheza vema dakika tisini za ugenini kumaliza kazi waliyoianza nyumbani.
“Dakika 90 za Afrika Kusini zilizobaki ndiyo kitu ambacho tunakiwaza sana hivi sasa, hakuna kingine zaidi ya hicho kwani tayari tuna matumaini ya kusonga mbele.
“Niwaambie Wanasimba kuwa safari hii hatutarudia makosa tuliyoyafanya msimu uliopita, kwa sasa tunaenda kamili gado tukiwa na akili timamu na uchungu mzito, hatutakubali kuwa ngazi ya wengine kwenda hatua ya nusu fainali.
“Tunaenda kutafuta nafasi ya kufuzu nusu fainali kwani matokeo yoyote ya ushindi tutakuwa tumevuka, tutakaporudi tutakuwa tupo nusu fainali tayari.”