Home Habari za michezo DABI YA WANAWAKE….YANGA PRINCESS ‘WAIKUNYUGA’ SIMBA QUEENS…WAFUTA UTEJA…

DABI YA WANAWAKE….YANGA PRINCESS ‘WAIKUNYUGA’ SIMBA QUEENS…WAFUTA UTEJA…

Baada ya Yanga Princess kucheza mechi sita kwa misimu tofauti bila kupata ushindi mbele ya watani zao Simba, leo imefuta uteja huo kwa kushinda bao 1-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Yanga imevunja uteja kwa Simba leo, na kupata ushindi wa kwanza baada ya kufungwa mechi tano na kuambulia sare moja kwenye michezo sita iliyopita.

Hata hivyo
ukiondoa suluhu ya msimu uliopita, mchezo huu wa leo ndio umeruhusu mabao machache kwani hapo awali Simba iloshinda 7-1, 5-1, 3-0, 3-1 na mara ya mwisho timu hizo zilipokutana ikashinda 3-0.

Aidha ushindi huo wa Yanga leo umevunja rekodi ya Simba kutopoteza mchezo kwenye kwa msimu kwani ilishinda mechi 14 zote za mwanzo.

Mchezo huo ulianza kwa timu zote mbili kucheza kwa kasi ya kawaida na dakika ya tano, Simba ilipata pigo baada ya beki wake Jullieth Singano kuoneshwa kadi nyekundu moja kwa moja.

Kadi hiyo Singano aliipata baada ya kumchezea rafu ya makusudi mshambuliaji wa Yanga, Clara Luvanga aliyekuwa anaenda kuleta madhara kwenye goli lao.

Baada ya hapo Yanga ilitumia mapungufu hayo kama faida kwao kwa kumiliki mpira kwa kiasi kikubwa na dakika ya 44 ilipata bao la kwanza kupitia kwa Luvanga aliyefunga kwa shuti kali iliyonshinda kipa wa Simba, Gelwa Yonah kudaka.

Bao hilo lilidumu hadi kumalizika kwa dakika 45 za kwanza na kipindi cha pili kilirejea kwa Simba kufanya mabadiliko mawili ya kiufundi yaliyoongeza kasi ya mchezo kwa upande wao.

Burudani zaidi kwenye mchezo huo ilikuwa eneo la kiungo walipokuwa wakicheza kiufundi, Amina Bilaly na Ireen Kisisa kwa Yanga huku kwa Simba wakicheza Joelle Bukuru na Pambani Kuzoya.

Timu zote ziliendelea kushsmbuliana kwa kupokezana huku zikitengeneza nafasi ambazo washambuliaji wa Simba na Yanga walishindwa kuzitumia vyema kufunga mabao na kufanya mechi hiyo imalizike kwa matokeo ya 0-1.

Matokeo hayo yameifanya Yanga kufikisha pointi 35 baada ya mechi 15 na kubaki nafasi ya tatu kwenye msimamo nyuma ya kinara Simba yenye alama 42 ikifuatiwa na Fountain Gate yenye 38 nafasi ya pili.

SOMA NA HII  BALAAH HILI....!! GWIJI GENK AMKATAA SAMATTA HADHARANI...AFUNGUKA A-Z JINSI TIMU ITAKAVYOYUMBA...