Home Habari za michezo POGBA ASHINDILIA MPANGO WA KUSEPA MAN UNITED…’KALEFT GRUPU’ LA WHATSAPP LA WACHEZAJI…

POGBA ASHINDILIA MPANGO WA KUSEPA MAN UNITED…’KALEFT GRUPU’ LA WHATSAPP LA WACHEZAJI…


KILA chenye mwanzo, kina mwisho. Paul Pogba amebonyeza kitufe kilichoandikwa ‘exist group’ akijiondoa kwenye kundi la WhatsApp la wachezaji wa Manchester United ikiwa ni maandalizi yake ya kuachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu, imeripotiwa.

Kiungo huyo Mfaransa ni kama vile ameshamalizana na Man United kwa kucheza mechi yake ya mwisho wakati alipoumia na kutolewa uwanjani mapema katika kipute cha kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Liverpool wiki iliyopita.

Pogba, 29, mkataba wake utafika tamati mwisho wa mwezi wa Juni na amegomea ofa ya kuongeza dili jipya la kuendelea kubaki Old Trafford.

Kwa mujibu wa gazeti la Mirror amewaambia wachezaji wenzake kwamba anaondoka zake mwishoni mwa msimu. Na anaonekana kuanza mpango wa kuachana na maisha ya Old Trafford kwa kujitoa kwenye kundi la WhatsApp la wachezaji wa klabu hiyo.

Pogba ameripotiwa kupokea ofa kutoka Real Madrid na Paris Saint-Germain, ambao wanachuana kuwania saini ya staa huyo anayejiandaa kuondoka Man United.

Kiungo huyo Mfaransa ni mmoja kati ya mastaa watatu wa bure ambao Real Madrid imelenga kuwasajili kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi, huku wengine wakiwa Antonio Rudiger na Kylian Mbappe.

Pogba uhusiano wake na mashabiki wa Man United umetibuka, ambapo hivi alikumbana na kelele za kuchomewa kwenye mechi ya ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Norwich City, ambayo bila ya shaka itakuwa ni mechi yake ya mwisho kucheza Old Trafford.

Baadaye alijaribu kuwapoza mashabiki hao kwa kutuma ujumbe kwenye Twitter baada ya kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Arsenal, alipoandika: “Najisikia vibaya kushindwa kuisaidia timu katika mechi ya leo. Napambana nirudi uwanjani nikiwa na nguvu mpya na natumaini nitafanya hivyo kabla ya msimu kumalizika.

“Mambo hayajaisha. Nawashukuru kwa sapoti yetu, kwa umoja tumesimama!”

Lakini, staa huyo hakuweza kificho kuhusu hafurahii maisha huko Man United wakati alipofichua hilo akiwa na chama la kimataifa la Ufaransa mwezi uliopita.

Staa huyo aliyeichezea Les Bleus mara 91, alisema: “Ni rahisi nikiwa na Ufaransa, ninacheza na nacheza kwenye nafasi yangu. Nafahamu wajibu wangu na najisikia kuaminiwa na kocha na wachezaji wengine. Ni rahisi kuwa tofauti Man United kwa sababu ni ngumu kucheza kwenye kiwango kilekile kama unabadilishwa nafasi yako, unabadilishiwa mfumo na unabadilishiwa mtu wa kucheza naye. Nitajua wajibu wangu kweli? Nimeuliza swali, lakini sina jibu.”

SOMA NA HII  JESSE LINGARD AIGOMEA MAN UNITED

Pogba alirudi kujiunga na Man United akitokea Juventus mwaka 2016 kwa ada ya Pauni 98 milioni. Na sasa ataondoka Old Trafford, huku klabu nyingine inayomsaka ni Barcelona, ambayo ina ukakika wa mkwanja baada ya kusaini dili la Pauni 236 milioni la udhamini wa Spotify. Staa mwingine anayesakwa na Barcelona ni supastaa wa Liverpool, Mohamed Salah.