Home Habari za michezo EDO KUMWEMBE: TATIZO SIMBA SIO WAVUMILIVU UGENINI…HATA WANGESHINDA 2-0 BADO WASIWASI UNGEKUWEPO…

EDO KUMWEMBE: TATIZO SIMBA SIO WAVUMILIVU UGENINI…HATA WANGESHINDA 2-0 BADO WASIWASI UNGEKUWEPO…


SHOMARI Kapombe alituliza kichwa juzi tena kwa mara nyingine na kufunga penalti pekee iliyoamua pambano la Simba dhidi ya Orlando Pirates katika uwanja wa Taifa pale Temeke. Mpaka sasa kocha wa Orlando, Mandla Ncikazi anaamini haikuwa penalti sahihi.

Vyovyote anavyoamini lakini Simba inakwenda nyumbani kwa Pirates wakiwa wanaongoza kwa bao moja. Lugha yoyote duniani ya kuelezea ushindi huu katika aina hizi ya mechi za mtoano huwa tunasema kwamba wanakwenda Soweto na ushindi mwembamba.

Miaka 19 iliyopita walikwenda Cairo Misri wakiwa na ushindi wa namna hii. Wale wanaume wa wakati ule walipambana kweli kweli. Wakafungwa bao moja tu na Zamalek. Mechi ikaenda katika matuta halafu Christopher Alex Massawe akafunga penalti ya mwisho iliyoacha mitaa mingi ya Tanzania ikiangua vilio tofauti.

Na sasa, katika nchi tofauti, watu wa rangi tofauti, michuano tofauti, Simba wanalazimika kurudia walichokifanya. Hata hivyo wanahitaji ushujaa mara mbili ya ule wa Cairo. Rekodi nyingi hazipo upande wao katika miaka hii.

Pablo Gomes atakwenda kufanya nini Soweto? Kusaka bao la ugenini? Kule Ulaya limeondolewa lakini Afrika bado lipo. Pablo atasaka bao la ugenini Soweto na hivyo kumaliza mechi au atatengeneza mistari miwili yenye nidhamu mbele ya Aishi Manula na kulipeleka pambano suluhu mpaka dakika 90?

Nina mashaka na hili jambo la pili. Simba sio wavumilivu ugenini. Katika miaka ya karibuni, makocha wamebadilika, kikosi kimebadilika kiasi lakini bado tabia ya timu uwanjani katika mechi za ugenini imekuwa ile ile tu. Wanachapwa mabao mengi ugenini. Hapa ndio huwa inakatisha tamaa kidogo.

Hata kama Simba wangeshinda mabao 2-0 Taifa bado tungekuwa na wasiwasi na maisha ya ugenini. Wamefungwa mara nyingi mabao zaidi ya hayo ugenini. Dhidi ya Vita, dhidi ya Al Ahly, dhidi ya TP Mazembe, dhidi ya Kaizer Chiefs, dhidi ya Asec Mimosas majuzi. Tayari mifano ni mingi.

Kitu cha huzuni ni kwamba Simba wanalazimika kupambana mara mbili zaidi kwa sababu kuna nguvu itapungua kwao na kuongezeka kwa Pirates. Bernard Morrison atakosekana katika pambano hilo na ni pengo kubwa kwao. Huyu ni msumbufu anayeweza kusababisha chochote, popote, wakati wowote. Kama alivyosababisha penalti.

Lakini pia Pirates itawarudisha kikosini mastaa wake wawili hatari. Thembinkosi Lorch na Gabadinho Mhango. Sijui kwanini walikosekana Dar es salaam lakini hawa ni tishio jingine kwa Simba pale Soweto. Kocha Pablo asiwasahau katika mipango yake.

Lakini zaidi ni kwamba Pirates watacheza mpira wao halisi wa kasi na kushambulia. Mbele ya mashabiki 60,000 walicheza kwa tahadhari kubwa lakini wakiwa kwao, mbele ya mashabiki wao watafungua pampu na kucheza kwa kasi zaidi. Ni hapo ambapo Simba watahitaji kuwa wavumilivu kwa dakika zote 90.

SOMA NA HII  YANGA WAFANYA KIKAO CHA SIRI NA WACHEZAJI...GAMONDI;- "SISI SIO MASHABIKI...AMEFUNGUKA HAYA

Kama pambano la Cairo limepita miaka mingi basi tunaweza kujikumbusha uvumilivu wa wachezaji wa Atletico Madrid katika pambano la wiki mbili zilizopita dhidi ya Manchester City pale Etihad. Walitengeneza mistari miwili na kuwa wavumilivu wa pasi za City na kasi yao. Walijisahau sekunde mbili tu ndipo Kelvin De Bruyne akawafunga.

Labda katika nyakati hizi za uvumilivu Simba wanaweza pia kufanya mashambulizi ya kushtukiza kuelekea katika lango la Pirates.

Hivi ndivyo mechi kubwa zinavyochezwa. Tatizo wakati mwingine Simba wanacheza mechi kubwa kama wapo nyumbani. Wanajaribu kupishana na wakubwa kila mara wakiwa ugenini.

Simba huwa wanafungwa mabao ya aina mbili wanapokuwa nje. Kwanza ni yake ya kukosa umakini wa kawaida lakini pili ni mpira ya kutengwa. Kuanzia kona na faulo. Ni mambo mawili ambayo Pablo analazimika kuyafanyia kazi kwa kiasi kikubwa.

Faida kwa Simba inaweza pia kurudi kwa Josh Onyango ambaye anabakia kuwa mlinzi namba moja wa kati katika kikosi cha Simba.

Mechi za namna hii zinahitaji wachezaji shupavu kama yeye ingawa anahitajika kuwa kiongozi zaidi uwanjani. Wakati inapofungwa mabao mengi ugenini na yeye anakuwepo uwanjani.

Inabidi alete nguvu mpya baada ya kukosa pambano la juzi.

Simba waende Soweto na umakini mkubwa. Zaidi wakumbuke kwamba katika hatua hii hawajawahi kuwafurahisha Watanzania. Wamekuwa wababe wanaoweza kupenya hatua ya makundi, lakini wakitoka katika makundi kwenda mtoano maisha yanakuwa magumu kwao.

Katika makundi Simba wanapata nafasi za kujitafakari kwa kiasi kikubwa.

Unaweza kujivunia kushinda mechi tatu za nyumbani na wakati mwingine hata ukipoteza tatu za ugenini unaweza kusonga mbele. Katika mtoano maisha hayawi hivi tena.

Wakati Simba walipokuwa katika kundi la AS Vita, Al Ahly na JS Saoura waliweza kuutumia vyema uwanja wa nyumbani na kushinda mechi zote tatu za nyumbani. Lakini wakafungwa mechi zote tatu za ugenini. Kama kila mechi ingekuwa ya mtoano, basi Simba angetolewa kwa sababu alishinda machache nyumbani akafungwa mengi ugenini.

Ni kesi ya msimu huu pia. Simba angekuwa amemtoa Gendarmerie tu. Angekuwa ametolewa na Berkane na Asec Mimosas kama mechi zingekuwa zinachezwa katika hatua ya mtoano. Jaribu kufikiria namna ambavyo alifunga mabao mengi dhidi ya Kaizer Chiefs, lakini ukweli ni kwamba alikuwa amefungwa mengi zaidi ugenini.

Makala haya yameandikwa na Edo Kumwembe na Kuchapishwa awali kwenye wavuti la MwanaSpoti.