Home Habari za michezo OSCAR OSCAR – “SIKUSHANGAA SIMBA KUSHINDA DHIDI YA ORLANDO…NILISHANGAZWA NA MASHABIKI WA...

OSCAR OSCAR – “SIKUSHANGAA SIMBA KUSHINDA DHIDI YA ORLANDO…NILISHANGAZWA NA MASHABIKI WA YANGA..”.


KWANZA matokeo! Yalinishtua? Lazima jibu langu liwe hapana. Ningeshtuka kama Simba wangeshinda kwa idadi kubwa ya mabao, labda kama tatu au nne lakini Ushindi wa moja bila nyumbani haushitui.

Wamefanya hivyo mara kadhaa dhidi ya bingwa wa Afrika, kivipi leo nishituke wakifanya hivyo dhidi ya timu ambayo haijanusa taji la Afrika kwa miaka Zaidi ya 20?

Lakini ningeshituka kama Simba angelazwa na Orlando Pirates kwasababu sijawazoea wakipoteza katika dimba la Mkapa. Sijawazoea wakipoteza mechi za kimataifa walizozipa uzito kama ambavyo waliwapa uzito Orlando Pirates. Bado naendelea kuamini kwamba wale Jwaneng wasingetamba siku ile kama Simba wangeipa mechi uzito kama ambavyo hufanya dhidi ya wakubwa wa Afrika. Huu ni ukweli ambao Simba hawawezi kuukubali hadharani.

Kama matokeo hayakunishitua, kipi basi kilinishitua? Kwanza kikosi cha Simba alichokianzisha kocha Pablo Franco. Alianza na mabeki wanne kama kawaida kisha katikati alianza na viungo wawili wazuiaji.

Kisa? Alikuwa muoga! Aliwaogopa Orlando Pirates kiasi cha kuanza na wachezaji sita katika eneo la ulinzi, hiyo ilimaanisha alikuwa na wachezaji wanne pekee katika eneo la ushambuliaji.

Matokeo yake timu ilishindwa kutengeneza nafasi nyingi za kufunga. Nakumbuka vema hadi wanaenda mapumziko Simba walikuwa wamepiga shuti moja tu lililolenga lango, tena lilitokana na umahiri wa Bernard Morrison na si mpango wa timu.

Nafikiri hii ni mechi ambayo Simba walipaswa kwenda kushambulia na kukazana kufunga mabao mengi kadiri wawezavyo hivyo kocha alipaswa ‘kubalansi’ mzani wa washambuliaji na wazuiaji. Sikuona sababu ya kuanza na wachezaji saba (tukimjumuisha na kipa) eneo la ulinzi.

Kwa asili ya soka la Afrika ilikuwa rahisi kutabiri kwamba Orlando watakuja kuzuia kuliko kushambulia, kikosi kile kilichoanza Kwa Mkapa unaweza kuanza nacho ugenini kwasababu unahitaji kuzuia zaidi, si nyumbani unapohitaji matokeo.

Nilishangaa zaidi Simba walipoamua kulinda baada ya kupata bao la kuongoza kupitia kwa Shomari Kapombe. Hata mabadiliko mwalimu aliyoyafanya baada ya bao yalilenga zaidi katika kulinda bao lao moja kuliko kuendelea kutafuta bao la pili, sikuelewa sababu ya msingi.

SOMA NA HII  PAMOJA NA BARBARA KUTIMKA SIMBA....HAYA HAPA MAMBO MAZITO ALIYOYAFANYA KWA MIAKA MIWILI TU.....

Ngoja kwanza Simba walipata bao baada ya kumpunguza kiungo mzuiaji mmoja na kumuweka kiungo mshambuliaji, alipotoka Taddeo Lwanga na kuingia Rally Bwalya Simba ilitengeneza nafasi zaidi za kufunga. Kwanini baada ya kufunga kocha akarudi tena kwa wazuiaji wengi? Ni uoga tu.

Kando ya mechi lipo lingine lililonishitua kidogo, nilikuwa uwanjani na sikuona kabisa mashabiki wa Yanga, labda kwasababu nilikuwa nimeketi lile jukwaa la watu watulivu wanaoketi nyuma ya mlango unaotumiwa na wachezaji kuingia uwanjani.

Lakini kijana wangu mmoja aliniambia hata kule mzunguko Yanga hawakutokea kama kawaida yao. Walikuwa wachache sana kiasi ambacho hawakujaza hata ‘nusu ya robo’ ya robo jukwaa, ungeweza kuwahesabu kwa haraka na kuimaliza idadi yao.

Hawa siyo Yanga niliowazoea. Katika mechi za kimataifa za Simba mara zote wanakuwa mashabiki wa wapinzani wa Simba ndani ya jezi zao za njano, sijui nini kiliwakumba juzi, tena haya yanatokea Yanga ikiwa inafanya vema katika mechi zake za nyumbani. Nilipata wazo ambalo hadi sasa silinunui, labda Yanga wanaifurahia timu yao kiasi ambacho kushinda kwa Simba hakuwaumizi. Sidhani kama ni kweli.

Pengine wanakereka Simba wanapowasimanga kwamba wao ni ‘kitengo mapokezi’ na mara zote huondoka uwanjani na aibu, sina uhakika na jibu langu lakini mashabiki wa Yanga kufika kwa uchache ule katika mechi ngumu ya Simba inashitua.

Niliporudi nyumbani nilikutana na hadithi nyingine ya kushitua, eti kulikuwa na mechi ya Ligi Kuu Bara kule makao makuu ya nchi kati ya Dodoma Jiji na Mtibwa Sugar. Mechi ilipigwa muda mmoja na mechi ya Simba.

Hapo unakaa chini na kumfikiria aliyepanga ratiba na muda wa mechi, alifikiria nini? Kwamba yupo shabiki nchi hii ambaye ataacha kukaa mbele ya runinga yake atazame mechi ya Simba na Orlando kisha aende uwanjani kuitazama Dodoma na Mtibwa? Natamani nipate idadi ya mashabiki waliohudhuria ile mechi ili nizidi kushituka.

Makala haya yameandikwa na Oscar Oscar na kuchapishwa awali kwenye wavuti la MwanaSpoti.