Home Habari za michezo KISA USHIRIKI WA SIMBA KIMATAIFA…KLABU LIGI KUU ZAJIKUTA NA MSALA WA KUFA...

KISA USHIRIKI WA SIMBA KIMATAIFA…KLABU LIGI KUU ZAJIKUTA NA MSALA WA KUFA MTU…ISHU IKO HIVI…


UKIONA Simba inavyobadilisha ndege kila mara kwenye safari zake za mechi za kimataifa, iheshimu.

Sio Simba tu, hata vigogo wengine kama Yanga na Azam ambazo kwa miaka zaidi ya 10 zimekuwa zikibadilisha uwakilishi wa nchi, ziheshimiwe.

Ipo hivi. Ukiziondoa timu hizo pamoja na Namungo, klabu nyingine zote zilizobaki katika msimamo wa Ligi Kuu hazitamani hata kwa dawa ofa ya kucheza mechi za kimataifa.

Kila moja inalia kwamba ule ni mziki mwingine ambao hawana pumzi ya kutosha ya kuukabili, japo wanaishukuru Simba kwa kuipambania Tanzania ikapata ofa ya kuwakilishwa tena na timu nne kwa msimu ujao kimataifa.

Simba inayojiandaa kuikaribisha Orlando Pirates ya Afrika ya Kusini kwenye mechi ya mkondo wa kwanza wa hatua hiyo, Jumapili ijayo kabla ya kurudiana nao Aprili 24, imeifanya nchi kupata nafasi mbili za Ligi ya Mabingwa na mbili za Shirikisho.

Hata hivyo, kabla klabu wawakilishi hazijafaamika, tayari baadhi ya klabu zimeweka bayana zinahofia kukata tiketi ya CAF kutokana na hali mbaya ya kiuchumi ilizonazo.

Hii itakuwa mara ya tatu kwa Tanzania kupata nafasi hizo, japo utayari wa timu kupambana na kupata matokeo huwa hauridhishi kwa timu kutomudu gharama huku klabu nyingine zikishindwa kumudu ushindani.

Itakumbukwa, mwaka 2004, Mtibwa Sugar ilifungiwa miaka mitatu na kupigwa faini ya fedha kwa kutokwenda kurudiana na Santos ya Afrika Kusini katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mtibwa ilifungwa nyumbani mabao 3-0, hivyo kukwepa kwenda Sauzi ikihofia kupoteza muda na pesa, kabla ya kukutana na rungu hilo la CAF.

Biashara United msimu huu iliondoshwa mashindanoni baada ya kukwama kucheza mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Al Ahly Tripoli ya Libya ambayo imetinga robo fainali ikijiandaa kucheza ndugu zao, Al Ittihad.

Kutinga kwa Simba robo fainali kunaifanya Tanzania kupata tena nafasi hizo, huku dalili zikionekana wazi kwamba Simba na Yanga zitashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao kutokana na nafasi zilizopo kwenye msimamo wa Ligi Kuu huku pia zikiwa katika robo fainali ya ASFC.

Timu nyingine zilizopo kwenye nafasi nzuri ya kukata tiketi ya CAF msimu ujao ni; Azam, Namungo, Mbeya City, Kagera Sugar, Geita Gold, KMC, Polisi Tanzania, Ruvu Shooting na Dodoma Jiji zinazoweza kubebwa na mbeleko hiyo ya Simba.

Hata hivyo, baadhi ya klabu zimeeleza hofu yao, licha ya kuona nafasi hiyo ni nzuri, lakini wanatamani kuikwepa kutokana na mzigo mkubwa wa gharama za ushiriki wa hatua za awali kabla ya kufika makundi ambako klabu hupata uhakika wa kuvuna mamilioni ya fedha.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA CHAMPIONI JUMATANO

Licha ya klabu kukiri uwepo wa nafasi hizo nne utaongeza ushindani kwenye Ligi Kuu Bara kama ilivyokuwa msimu uliopita, lakini wasiwasi unakuja juu ya utayari wa klabu kushiriki mashindano hayo hasa kwenye gharama na ubora wa vikosi vyao.

Viongozi wa klabu hizo kwa nyakati tofauti wameeleza wasiwasi wao katika ushiriki wa timu nne CAF, licha ya kuamini kwenye Ligi ushidani utaongezeka.

“Kufuzu ni suala moja na kushiriki na kushinda ni suala jingine, sasa tumepata nafasi nne, lakini je utayari wa timu zinazopata tiketi hiyo ukoje?” alihoji Ofisa Mtendaji Mkuu wa Namungo, Omary Kaya.

Kaya alikumbushia baadhi ya timu nchini zilivyokuwa gumzo, ikiwamo Biashara baada ya kupata tiketi hiyo msimu huu na kushindwa kuitumia vema.

Msimu ujao, timu tatu zitakazomaliza ligi kwenye nafasi ya juu na bingwa wa Kombe la Shirikisho (ASFC) msimu huu ndizo zitaiwakilisha nchi kimataifa.

Biashara iliondolewa mashindanoni baada ya kutofika kwa wakati nchini Libya kwenye mchezo wa marudiano Al Ahly Tripoli.

Hadi siku ya mechi, timu hiyo haikuwa na uhakika wa safari na kuomba mechi hiyo isogezwe, lakini CAF ikaigomea na kuiondosha.

Licha ya uongozi kudai changamoto ilianza kwa kukosa kibali cha kupita kwenye anga ya kimataifa nchini Sudan, Sudan Kusini na cha kutua Benghazi ulipokuwa uchezwe mchezo huo, habari za ndani zilidai, timu hiyo haikuwa na pesa za maandalizi ya safari kwaji haikujiandaa mapema.

“Hii ni rekodi ambayo tunaamini ina manufaa kwenye nchi, Simba tumekuwa na historia nzuri kimataifa, hivyo jukumu ni la timu zote zitakazopata nafasi hiyo kujipanga ili zifaye vizuri zaidi,” alisema Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ akielezea jinsi timu hiyo ya Msimbazi inavyoibeba nchi kimataifa.

Historia inaonyesha mbali na Mtibwa, timu za KMC, Biashara na Namungo zimeshiriki mashindano hayo zikiwa na changamoto kadha wa kadha, hasa katika pesa na ubora wa vikosi, huku wababe Simba, Yanga na Azam zikishiriki kwa kiwango chao.

Namungo yenyewe iliishia hatua ya makundi katika mashindano ya kimataifa, ikiwa haijashinda mechi hata moja wala kufunga bao, japo ugeni wao uliwasaidia wasisakamwe sana, kwani ilishiriki kwa mara ya kwanza na kusapraizi kufika hatua ya makundi.

Mwaka 2019, KMC iliondoshwa mapema kwenye mashindano ya kimataifa baada ya kufungwa nyumbani mabao 2-1 na AS Kigali ya Rwanda ikiwa ni mara ya kwanza.