Home Habar za Usajili Simba USAJILI SIMBA…THEDEO LWANGA ‘OUT’…KIUNGO MNIGERIA MKATA SHOMBO ‘IN’…DILI ZIMA LIKO HIVI AISEE…

USAJILI SIMBA…THEDEO LWANGA ‘OUT’…KIUNGO MNIGERIA MKATA SHOMBO ‘IN’…DILI ZIMA LIKO HIVI AISEE…


RASMI sasa kiungo mkabaji wa Coastal Union ya mkoani Tanga, Mnigeria, Victor Akpan, anakuja kuchukua nafasi ya Mganda Taddeo Lwanga katika usajili wa msimu wa 2022/2023.

Mnigeria huyo katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba, ndiye alikuwa tishio kwa Coastal wakati timu hizo zilipovaana wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga huku akimtungua Aishi Manula bao la kiufundi la mita 20.

Kiungo huyo amekuwa akionyesha ubora mkubwa wa kutoa pasi za mbali na kufunga mabao ya mbali pia.

Simba ipo katika mipango ya kuachana na Lwanga mwenye majeraha mwishoni mwa msimu huu baada ya mkataba wake wa miaka miwili kumalizika.

Mmoja wa viongozi kutoka ndani ya uongozi wa Simba, ameliambia Championi Jumatatu kuwa timu hiyo wataachana na Lwanga kutokana na majeraha ya muda mrefu ya goti ambayo ameyapata mwanzoni mwa msimu huu.

Kiongozi huyo alisema kuwa upo uwezekano mkubwa wa Akpan kupewa mkataba wa miaka miwili ya kuichezea timu hiyo, mara baada ya kufikia makubaliano mazuri kati ya uongozi na mchezaji.

Aliongeza kuwa kiungo huyo amependekezwa katika usajili baada ya kuvutiwa na kiwango chake kikubwa ambacho amekionyesha katika michezo ya ligi nyumbani na ugenini.

“Lwanga hayupo kabisa katika mipango yetu ya usajili msimu ujao, ni baada ya baadhi ya viongozi wa benchi la ufundi kupendekeza kuachwa ili apatikane mwingine mwenye kiwango bora.

“Na mchezaji anayepigiwa hesabu ni Akpan ambaye yeye hahitaji kuangaliwa kwa maana ya kufanyiwa majaribio, kwani benchi la ufundi limeuona uwezo wake.

“Yapo mazungumzo ya awali yanayofanywa hivi sasa kati ya kiungo huyo na uongozi, kama dili hilo litafikia pazuri basi atasajiliwa Simba msimu ujao,” alisema kiongozi huyo.

Alipotafutwa Akpan kuzungumzia hilo, alisema: “Mapema kuzungumzia hatima yangu ya msimu ujao, licha ya kuwepo mazungumzo na baadhi ya klabu za hapa nchini zilizonifuata kwa ajili ya mazungumzo.

“Kingine muda wa usajili bado, hivyo tusubirie na kingine mimi bado mchezaji halali wa Coastal niliyebakisha mkataba wa mwaka mmoja, hivyo timu itakayonihitaji kwanza ifanye mazungumzo na klabu yangu.”

SOMA NA HII  JEMEDARI SAID:- KWA HILI LA NTIBAZONKIZA....TFF WAMEJITIA AIBU MNOOO...