Wakati mashabiki wakisubiri kwa hamu mchezo wa kesho wa Ligi kuu kati ya Dodoma Jiji na Yanga, Kocha wa Yanga, Nesreddine Nabi amedai sehemu ya kuchezea ya uwanja wa Jamhuri sio nzuri.
Yanga inahitaji ushindi katika mchezo huo ili kuongeza gepu la pointi dhidi ya Simba ikiwa ni sehemu ya mbio za ubingwa msimu huu
Timu hiyo inaongoza Ligi ikiwa na pointi 57 huku Dodoma Jiji wao wakiwa nafasi ya nane na pointi 28 ambapo mechi iliyopita dhidi ya Polisi Tanzania walitoka suluhu ugenini dhidi ya Polisi Tanzania mjini Moshi.
Yanga mchezo wa mwisho ilitoka suluhu na Tanzania Prison kipute kilichofanyika katika uwanja wa Mkapa jijini Dar es salaam.
Mchezo wa mzunguko wa kwanza Dodoma Jiji walikubali kichapo cha mabao 4-0 mtanange uliofanyika uwaja wa Mkapa.
Akizungumza na waandishi wa wabari jana Mei 14 jijini hapa, Nabi amesema: “Lakini kesho tunaweza kucheza mechi mbili tunacheza na Dodoma Jiji lakini pia tunacheza dhidi ya uwanja tunajua kwamba viwanja haviwezi kufanana na Mkapa, Mbeya ama Morogoro lakini kuna changamoto za uwanja.”
Amesema kuna haja wanaohusika kuliangalia jambo hilo kwani ligi inafuatiliwa na watu wengi.
“Ni lazima miaka ya mbele tuangalie miundombinu ya viwanja,” amesema.