BEKI na Nahodha wa Yanga Bakari Mwamnyeto ataendelea kubaki ndani ya klabu hiyo kwa miaka mingine miwili.
Mwamnyeto amesaini dili hilo leo jioni mbele ya wafadhili wa Yanga GSM mkataba huo ambao sasa utamfanya kuitumikia klabu hiyo kwa jumla ya miaka minne.
Meneja wa beki huyo wa zamani wa Coastal Union Kassa Mussa amezungumza akiwa Italia akithibibitisha hatua hiyo.
“Tumeamua kubaki Yanga kwa kuwa ni klabu ambayo tumekubaliana na kijana wangu (Mwamnyeto) kubaki baada ya kuona mafanikio mazuri katika mkataba wa kwanza” amesema Kasa.
Tangu atue Yanga Mwanyeto amekuwa na mafanikio makubwa ndani ya klabu hiyo akijihakikishia nafasi katika kikosi cha kwanza huku pia akipewa unahodha ndani ya klabu hiyo kongwe.
Hatua hiyo inaifanya Yanga kushinda vita muhimu kufuatia watani wao Simba na Azam kuwa katika mbio za kuwania saini ya beki huyo wa zamani wa Coastal Union.