Rais Samia Suluhu Hassan leo Mei 31, 2022 amepokea kombe la Dunia Ikulu jijini Dar es Salaam ambalo litakaa kwa siku mbili nchini kabla ya kuondoka.
Kombe hilo amekabidhiwa na mchezaji mkongwe wa Brazil Juliano Belletti ambaye anaongoza timu katika ziara ya kombe hilo nchini.
Akipokea kombe hilo Rais Samia amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kesho Juni 1, 2022 kufika Uwanja wa Taifa wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam kupiga picha na kombe hilo.
Tanzania inakua miongoni mwa nchi tisa za Afrika ambazo imepata bahati ya kupitiwa na kombe hilo.
Samia amefafanua kuwa Tanzania imechaguliwa kuwa miongoni mwa nchi hizo kutokana na kuendelea kufanya vizuri kwenye michezo ambapo amesema watanzania wengi wanapenda soka.
Kesho kombe litaanza kuonyeshwa kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 11 jioni na baada ya hapo itaonyeshwa filamu ya Royal tour.
Rais ametoa rai kwa watanzania kutumia ujio wa kombe la Dunia nchini kuitangaza Tanzania duniani.
Kwa upande wake, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa amemshukuru Rais kwa kufanya mapinduzi makubwa kwenye michezo katika kipindi kifupi cha utawala wake.