Home Habari za michezo ALICHOSEMA EDO KUMWEMBE BAADA YA YANGA KUMUONGEZEA MKATABA MAUYA…”MUKOKO ALILIONA.. AKAMUA KUONDOKA”….

ALICHOSEMA EDO KUMWEMBE BAADA YA YANGA KUMUONGEZEA MKATABA MAUYA…”MUKOKO ALILIONA.. AKAMUA KUONDOKA”….


NILIPOSOMA mahali kwamba Yanga wamemuongezea mkataba wa miaka miwili, Gift Mauya nimekumbuka mambo mengi. Nimekumbuka tabia za wachezaji wetu. Nimekumbuka kuandika kitu kwa ajili ya kumpongeza. Sio kila wakati tuwe tunaandika kwa ajili ya kuponda.

Wachezaji wa kigeni huwa wanasifiwa zaidi kuliko wachezaji wazawa lakini nichukue nafasi hii kumpongeza Gift. Haikuwa kazi rahisi kwake. Aliwasili klabuni hapo miezi 24 iliyopita akitokea Kagera Sugar. Alisajiliwa pamoja na mchezaji aliyeitwa Mukoko Tonombe ambaye alitokea Congo.

Mukoko alionekana kuwa kipenzi cha Wanayanga kwa sababu ya staili yake ya soka la kujituma. Wengine walimuita ‘Teacher’. Sijui ni kwa sababu gani walimuita hivyo lakini ukweli ni kwamba Mukoko alionekana kuwa mchezaji asilia wa Yanga kutokana na tabia yake ya kujituma.

Gift na Mukoko waliletwa Yanga kwa kile ambacho kilionekana kama vile kuungana na Fei Toto kwa ajili ya kutengeneza safu maridadi ya kiungo Yanga. Yanga walihisi kama miaka mitatu ambayo walikaa bila ya taji ilikuwa imetosha.

Katika timu Mukoko alionekana kujituma zaidi lakini ukweli ni kwamba Gift alionekana mzuri zaidi kwa kutulia na mpira mguuni. Wakati Mukoko akiingia katika nafsi za mashabiki wa Yanga, Gift aliingia katika nafsi za mashabiki wa Yanga baada ya bao lake pekee kuizamisha Simba katika pambano la Ligi msimu uliopita.

Hata hivyo, msimu huu ulipaswa kuwa mgumu kwa Gift. Pale katikati yeye na Mukoko waliletewa watu wawili mwanzo wa msimu. Khalid Aucho na Yannick Bangala. Suala lilikuwa ni nani anaweza kuangukia chaguo la tatu katika eneo la kiungo sehemu ya nyuma.

Feisal alikuwa salama kwa sababu kocha wake alimhamishia mbele. tatizo lilikuja kwa Mukoko na Gift kwa sababu mafundi wawili walichukua nafasi zao. Hatimaye Gift akajikuta akiangukia chaguo la tatu huku Mukoko akiwa chaguo la nne.

Yanga walikuwa wanapitia mabadiliko mengine ya kitimu. Wakati Gift na Mukoko waliimarisha Yanga katika eneo la kiungo, Aucho na Bangala waliipeleka Yanga katika hatua nyingine. Suala la Mukoko kuwa chaguo la nne lilikuwa wazi zaidi.

Ukiwatazama Gift na Mukoko ni wazi kwamba Gift alionekana kuwa na kipaji zaidi. Tofauti ni kwamba Mukoko alikuwa anajituma zaidi lakini ukweli ni kwamba Gift alikuwa na kipaji asilia kuliko Mukoko. Haikushangaza kuona Gift anaangukia kuwa chaguo la tatu halafu Mukoko anakua chaguo la nne.

Hata hivyo, kuna watu wa Yanga waliwahi kuninong’oneza kwamba Gift alionekana kukata tamaa wakati alipoanza kuwekwa benchi na nafasi yake kuchezwa na Bangala na Aucho. Hapo ndipo kulikuwa na mstari mwembamba kati ya kuachwa na Yanga au kupambana na kupata mkataba mpya.

Bahati yake ni kwamba kuna nyakati ambazo mmoja kati ya walinzi wa kati, kati ya Bakari Mwamunyeto na Dickson Job angeweza kukosekana. Yannick Bangala alirudi kucheza kama mlinzi wa kati na Gift alicheza kando ya Aucho.

Gift alionekana kumudu kucheza vema na fundi Aucho huku Mukoko akiwa benchi. Hapana shaka Mukoko aliliona hili na ndio maana akaamua kufungasha virago vyake na kuondoka. Hata watu wa Yanga waliona unafuu kwa Mukoko kuondoka kwa sababu wangeitunza nafasi moja ya mchezaji wa kigeni kwa matumizi ya siku za usoni.

SOMA NA HII  SABABU YA FEI KUMWAGA MACHOZI BAADA YA KUGAWANA POINTI NA KAGERA SUGAR

Lakini hapo hapo Mukoko alikuwa hatazamwi vema na baadhi ya viongozi wa Yanga tangu alipompiga John Bocco kwa makusudi kwenye uwanja wa Lake Tanganyika pale Kigoma katika pambano la nusu fainali michuano ya FA. Wanaamini aliihujumu timu.

Kucheza kama kiungo wa tatu msaidizi kulimsaidia Gift kwa kiasi kikubwa. Lakini zaidi ni kwamba ameimarika kwa sababu anacheza na mafundi. Lakini hapo hapo kitendo cha Bangala kuendelea kuitendea haki nafasi ya ulinzi kumemsaidia Gift kupata nafasi ambayo hakuitarajia.

Amejitahidi kwa kiasi kikubwa kuwashawishi watu wa Yanga waendelee kumuamini. Ni wachezaji wachache wa Tanzania ambao wangeendelea kukaza. Wengine wangeishia kumlaumu kocha na kulalamika katika vyombo vya habari kwamba wanaonewa.

Pale Simba kuna wachezaji wa namna hii ambao wameendelea kunifurahisha. Wachezaji wa kizawa ambao wameamua kupambana licha ya kuwepo kwa mastaa wengi wa kigeni katika nafasi zao. Achilia mbali Mohamed Hussein Tshabalala na Shomari Kapombe ambao nafasi zao zinaonekana kuwa salama kwa sababu wasaidizi wao ni wazawa, lakini Jonas Mkude, Hamis Dilunga na John Bocco wamekuwa wakipambana na wageni.

Jonas amecheza sambamba na James Kotei, Fraga na sasa Thadeo Lwanga. Hata hivyo, bado anapambana tu. licha ya wakati mwingine kulega hapa na pale kutokana na tabia zake binafsi kutokuwa nzuri lakini Jonas anafanya kile ambacho Gift kwa sasa anajaribu kufuata nyayo.

Dilunga naye amekuwa akipambana na wageni. Nafasi yake kulikuwa na mafundi wengi kina Luis Miquissone, Bernard Morrison na hata Clatous Chama ambaye wakati mwingine amekuwa akitokea pembeni. Hata hivyo, Dilunga ameendelea kuwa imara katika nafasi yake. Ni kama ambavyo John Bocco ameendelea kupambana na Chris Mugalu na Meddie Kagere katika ufungaji.

Ujumbe mmoja ni kwamba Waingereza waliamua kunyoa au kusuka. Waliamua Ligi yao iwe na mvuto zaidi kwa kuruhusu wachezaji kutoka mataifa mbalimbali kwenda kwao na kucheza. Sisi hatuwezi kuwalinda wachezaji wetu kwa kuwaondolea ushindani kama Mzee Harrison Mwakyembe alivyowahi kushauri.

Hawa kina Mauya inabidi wazitolee jasho nafasi zao hata wanapoletewa wachezaji mafundi. Hawa kina Bangala na Aucho wamekuja kuwaonyesha kile ambacho wanapaswa kufanya uwanjani. Ni uamuzi wao kina Mauya kujifunza au kuwa na chuki.

Nadhani Gift ameamua kujifunza na kupambana. Ni jambo ambalo linaisaidia timu yake lakini pia linaweza kuisaidia timu ya taifa. Timu kubwa kama Simba, Yanga na Azam hazitaacha kuleta mastaa wa nje wenye vipaji vikubwa. Ni jukumu la kina Gift kupambana. Nashukuru ameamua kufanya hivyo kiasi cha kwamba Yanga wameamua kumuongezea mkataba mpya.

Makala haya yameandikwa na Edo Kumwembe na kuchapishwa awali kwenye wavuti la MwanaSpoti.