Home Habari za michezo WAKATI TETESI ZA KUWA KWENYE UGOMVI NA CHAMA ZIKIZIDI KUKUA…PABLO AIBUKA NA...

WAKATI TETESI ZA KUWA KWENYE UGOMVI NA CHAMA ZIKIZIDI KUKUA…PABLO AIBUKA NA KUSEMA HILI…


Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Franco Pablo Martin amekanusha uvumi wa kuwa na ugomvi na Kiungo Kutoka nchini Zambia Clatous Chotta Chama.

Wawili hao walidaiwa kuwa na ugomvi, baada ya kupishana kauli wakiwa kwenye chumba cha kubadilishia wakati wa mapumziko kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Young Africans Jumamosi (April 30), hatua ambayo ilipelekea Kocha Pablo kumtoa Chama na nafasi yake kuchukuliwa na Rally Bwalya.

Mbali na maamuzi hayo, pia ilidaiwa kuwa Kocha Pablo alifanya maamuzi ya kumuacha Chama Dar es salaam wakati timu yake ilipokwenda mkoani Lindi kucheza dhidi ya Namungo FC juzi Jumanne (Mei 03), kama sehemu ya adhabu ya kilichotokea Jumamosi (April 30).

Kocha huyo kutoka nchini Hispania amesema taarifa za kuwa na ugomvi na Chama sio za kweli, kwa sababu kila mchezaji wa Simba SC ana uhusiano mzuri na Benchi lake la Ufundi.

Amesema Chama aliachwa Dar es salaam wakati wa safari ya Mkoani Lindi, kutokana na matatizo ya kiafya (Homa), huku Morrison alikua ana matatizo binafsi ambayo hakuwa tayari kuyataja.

“Chama aliachwa kwa kuwa anasumbuliwa na homa na kwa Morrison alikuwa na ishu binafsi, hayo mengine yanayosemwa huko sijui yanatokea wapi.”

“Kila mchezaji wangu ana uhusiano mzuri sana na mimi kama Kocha Mkuu pamoja na wasaidizi wangu wote katika Benchi la Ufundi, haijawahi kutokea ugomvi kati yangu na yoyote kwenye kikosi.” amesema Kocha Pablo

Kocha Pablo bado anaendelea kupambana katika Michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, licha ya kuachwa kwa alama 13 na Young Africans inayoendelea kuongoza msimamo wa Ligi.

SOMA NA HII  WAKATI LIGI KUU IKIWA IMEISHA...HII HAPA REKODI MBAYA NA YA KIPEKEE ILIYOWEKWA NA INONGA....