Home Habari za michezo WAKATI WAKITAFUTA POINTI ZA UBINGWA….SHABANI DJUMA ‘OUT’ …KAZE AKAZIA JAMBO HILI YANGA…

WAKATI WAKITAFUTA POINTI ZA UBINGWA….SHABANI DJUMA ‘OUT’ …KAZE AKAZIA JAMBO HILI YANGA…


WAKATI ikihitaji pointi 11 tu katika mechi zake sita zilizosalia ili kutangazwa rasmi kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu Bara, Klabu ya Yanga Jumamosi itamkosa mkali wake wa pasi za mwisho, beki wa kulia, Shaban Djuma, itakapoikaribisha Mbeya Kwanza katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Yanga ambayo ipo kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 60 baada ya mechi 24, inahitaji alama 11 tu ili kufikisha 71, ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote kati ya 16 zinazoshiriki kinyang’anyiro hicho msimu huu.

Simba iliyopo nafasi ya pili ikiwa na pointi 49 zilizotokana na michezo 23, kabla ya mechi yake ya jana ugenini dhidi ya Azam FC, kama itashinda mechi zake zote ukiwamo wa jana (kama imeshinda), itafikisha pointi 70, moja nyuma ya Yanga endapo vinara hao watavuna alama 11 katika michezo yao sita iliyobaki.

Hata hivyo, kuelekea mchezo wa Jumamosi dhidi ya Mbeya Kwanza, ambao Yanga itakuwa ikipigana kufa au kupona ili kupata ushindi na kuendelea kujenga matumaini yao ya kutwaa ubingwa huo mapema kabla ya ligi kumalizika, itamkosa Djuma ambaye atakuwa nje ya uwanja akitumikia adhabu ya kadi tatu za njano.

Akizungumza na mwandishi wetu jana, Kocha Msaidizi wa Klabu ya Yanga, Cedric Kaze, alisema wanaendelea kujiandaa kwa mechi hiyo lakini watamkosa Djuma.

“Tunashukuru tunaendelea vizuri na mazoezi kwa ajili ya mchezo wetu ujao, tunamheshimu mpinzani wetu kwani msimu huu hakuna timu ya kuibeza.

“Tutaendelea na mazoezi leo jioni, kitu ambacho tunashukuru mpaka sasa hatuna majeruhi, isipokuwa tutamkosa mchezaji wetu Djuma Shaban, ambaye ana kadi tatu za njano, ila lengo letu la pointi tatu kwenye mchezo huo lipo palepale,” alisema.

Djuma amekuwa msaada mkubwa katika upishi wa mbao Yanga, kwani hadi sasa ni miongoni mwa wachezaji wanne wenye pasi za mwisho (‘assists’) nyingi (nne), kwenye ligi hiyo ambayo ipo raundi ya 24.

Mbali na Djuma, wachezaji wengine wenye ‘assists’ nne hadi sasa ni Pius Buswita wa Ruvu Shooting, Tepsi Evance (Azam FC), Christian Zigah (Biashara United) na Aboubakar Ngalema wa Dodoma Jiji FC.

SOMA NA HII  BAADA YA VYUMA VYA MAANA KUTUA YANGA....INJINIA HERSI AIBUKA NA HII MPYA....

Aidha, Kaze alisema lengo lao ni kuendelea kushinda ili kutwaa ubingwa huo msimu huu ambao wameukosa kwa misimu minne sasa.

“Msimu huu mikakati yetu ni kuchukua ubingwa na hilo litawezekana kwa kuendelea  kufanya vizuri katika michezo yetu iliyobaki,” alisema.

Baada ya mechi hiyo, Yanga itasafiri kwenye jijini Mwanza tayari kwa mechi yao ijayo dhidi ya Biashara United kabla ya kubaki katika jiji hilo ikiisubiri Simba kwa mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Soka nchini, FA Cup utakaopigwa Uwanja wa CCM Kirumba Mei 28,

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here