Simba imeachana na aliekuwa Kocha wake Mhispaniola Pablo Franco Martin wiki moja iliyopita baada ya kuondoshwa kwenye Kombe la ASFC hatua ya nusu fainali, lakini pia wakiwa na nafasi ndogo ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu.
Sasa tayari Simba wameshaanza mchakato wa kumsaka mrithi wa Pablo na Makocha kutoka sehemu mbali mbali wametuma CV zao wakiwania nafasi ya kukinoa kikosi hicho kwa msimu ujao.
Simba kwa sasa iko chini ya Kocha wake msaidizi Selemani Matola, na hii leo mtendaji Mkuu wa Simba Barbara Gonzales amedokeza mchakato huo ulipofikia;
“Tumepokea wasifu wa makocha zaidi ya 100 kutoka sehemu mbalimbali duniani ambao wengi wao ni kutoka barani Ulaya na Amerika Kusini. Mchakato wa mchujo unaendelea na tunategemea utakamilika ndani ya wiki mbili zijazo”
“Tunahitaji Kocha anayejua vizuri soka la Afrika pia tungefurahi kupata Kocha ambaye ni mzawa wa bara hili lakini mpaka sasa bado hawajatuma wasifu na aliteyuma mmoja na vigezo vyake havitoshi” amesema Barbara