Home Habari za michezo SIMBA YA MSIMU UJAO NI MOTO AISEE….WAPANIA KUMVUTA DIARRA KUTOKA ‘NG’AMBO’…ISHU NZIMA...

SIMBA YA MSIMU UJAO NI MOTO AISEE….WAPANIA KUMVUTA DIARRA KUTOKA ‘NG’AMBO’…ISHU NZIMA IMEKAA NAMNA HII…


WAKATI sekeseke la usajili likiendelea ili kupata wachezaji watakaoleta manufaa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, Simba imezidi kuingia vitani kunasa saini ya wachezaji mapro wapya.

Inaarifiwa kwamba Simba iko kwenye mchakato na kiungo wa Red Arrows ya Zambia, Mmali Allasane Diarra.

Taarifa kutoka ndani ya Simba zinaeleza hadi kikao cha mwisho kuhusu usajili wa msimu ujao, kilichofanywa chini ya Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez na aliyekuwa kocha wao Pablo Martin walikubaliana kuleta kiungo mshambuliaji mmoja wa kigeni.

Imeelezwa kuwa baada ya kukubaliana waliweka mezani majina ya viungo washambuliaji wanne, chaguo la kwanza hadi la nne na mmoja kati ya hao ndio asajiliwe.

Awali ilifahamika kuhusu viungo chaguo la kwanza hadi la tatu ambao ni Victorien Adebayor anayeweza kutua RS Berkane ya Morocco, Morlaye Sylla na Stephane Aziz Ki anayetajwa Yanga.

Lakini sasa Simba wamebaki na uhakika wa kumpata Diarra pekee kati ya hao anayecheza Ligi Kuu Zambia klabu ya Red Arrows iliyocheza na Simba hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika. Diarra ameingia katika orodha hiyo kutokana na kiwango chake bora alichoonyesha kwenye ligi yao, Kombe la Shirikisho ikiwemo mechi mbili dhidi ya Simba ambazo zote alianza.

“Unajua tumekubaliana kwenye kila nafasi moja tuliyopanga kusajili mchezaji mpya wa kigeni tumeweka chaguo la kwanza hadi la nne kulingana na viwango vyao vilivyo,” alisema bosi mmoja ndani ya Simba na kuongeza;

“Tumeamua kufanya hivyo ili kuweka nguvu kusajili mchezaji chaguo la kwanza kama tukishindwa tunashuka chini kwa maana chaguo la pili, tatu au nne na naamini tutafanikisha kumpata mmoja kati yao.”

Diarra aliyezaliwa Januari 8, 1997 amewavutia Simba kutokana na uwezo wake wa kumiliki mpira, kupiga pasi zenye kuanzisha mashambulizi, kufunga mabao na kuwasumbua viungo wa timu pinzani.

Simba imepanga kusajili kiungo mmoja wa ushambuliaji kutokana na kutokuridhishwa na kiwango cha Clatous Chama, Rally Bwalya ambaye dili lake la kutua Amazulu likikamilika anaweza kutimka ikiwemo viwango vya nyota wengine wa nafasi hiyo kutokuwa bora.

SOMA NA HII  MANULA AINGIA ANGA ZA MAMELODI SUNDOWNS

Wakati huo huo, Simba watakuwa na nafasi ya kuongeza wachezaji wa kigeni baada ya kuacha na Benard Morrison huku Pascal Wawa, Meddie Kagere na Taddeo Lwanga nao wanatajwa kutemwa mwishoni mwa msimu.

Kiungo wa Simba, Sadio Kanoute alisema aliwahi kucheza na Diarra kwenye ligi ya Mali pamoja na timu ya taifa ya vijana ni moja wa wachezaji wazuri.

“Sina shaka na Diarra naamini katika uwezo wake ni moja ya viungo wazuri washambuliaji ila kama kuna jambo lingine lolote sifahamu kwa maana sina mawasiliano nae ya mara kwa mara,” alisema Sadio.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ na Barbara kila mmoja kwa nafasi yake alizungumza kuwa timu hiyo itafanya usajili wa maana msimu huu.