UAMUZI wa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano na Usajili ya Yanga aliye pia Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said kuwania nafasi ya Urais wa klabu hiyo katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Julai 10 ndio habari iliyo gumzo kwa sasa.
Licha ya kundi kubwa la wanachama na mashabiki wa klabu hiyo wakiunga mkono kitendo cha Hersi kuwania nafasi hiyo ya Urais, baadhi wameonesha wasiwasi juu ya uamuzi huo.
Wasiwasi huo unatokana na hofu ya kuibuka kwa mgongano wa kimaslahi kwa Hersi ambaye amebaki mgombea pekee wa nafasi hiyo na nafasi aliyonayo ndani ya klabu na kampuni ya GSM ambayo yeye ni muajiriwa.
Mmoja wa vigogo wa Yanga, aliliambia gazeti hili anafahamu utendaji kazi wa Hersi na anaamini unaweza kuisaidia Yanga, iwapo ataibuka na ushindi lakini kinacholeta maswali ni nafasi yake ndani ya mdhamini wao GSM.
“Hakuna kosa kikatiba kwa Hersi kugombea na ni mtu ambaye Wanayanga wengi tunamkubali kutokana na kujituma kwake. Lakini changamoto kubwa ni suala la mgongano wa kimaslahi. Yule ni mwajiriwa wa mdhamini ambaye anaweza kuwa mwekezaji. Rais atapaswa kusimamia hisa za klabu lakini kumbuka atapaswa pia kusimamia maslahi ya mwajiri wake.”
“Tunahitaji kuondolewa ukakasi katika hili kwa maslahi mapana ya klabu pamoja na mdhamini,” alisema kigogo huyo.
Mwanachama wa Yanga, Christopher Kashililika alisema klabu hiyo inapaswa kuepuka kilichotokea kwa watani wao Simba.
“Mchakato huu umesimamiwa na mdhamini na leo mkurugenzi kutoka upande wa mdhamini ameonyesha nia ya kuwania Urais. Ni haki yake kikatiba kwa sababu ni mwanachama wa Yanga lakini tunapaswa kuwa makini kuepuka migogoro inayotokea upande wa Simba ambao mwekezaji alisimamia mchakato wa mabadiliko na baadaye akawa sehemu ya uongozi,” alisema Kashililika.
Hata hivyo wakati baadhi ya wanachama wakionyesha wasiwasi huo, kundi kubwa linaonekana kumsapoti Injinia Hersi na miongoni mwao ni Makamu wa Mwenyekiti anayemaliza muda wake, Fredrick Mwakalebela ambaye juzi alitamka hadharani kumuunga mkono mgombea huyo.
Hatuwezi kuwaacha Wanayanga kama watoto yatima ndio maana nimekuja kuunga mkono za Eng. Hersi Said kugombea nafasi ya Urais Yanga SC, alisema Mwakalebela.
MASWALI MATANO YANAYOFIKIRISHA
1. Rais wa klabu ndiye anayesimamia hisa 51% za upande wa wanachama. Ikitokea Injinia Hersi ameshinda na mwajiri wake akawa mmoja wa wawekezaji, atasimamia pia za upande wa mwekezaji ambako yeye ni Mkurugenzi wa Uwekezaji au atajiondoa upande alikoajiriwa?
2. Je, uchaguzi unafuata misingi ya usawa, uwazi na haki ukizingatia mmoja kati ya waliojitokeza kuwania urais alishiriki kwa kiasi kikubwa kusimamia mchakato wa mabadiliko?
3. Kutakuwa na mazingira ya usawa katika uingiaji wa mikataba ya udhamini kwa kampuni na taasisi nyingine mbele ya mdhamini wa sasa pindi mwajiriwa wake akifanikiwa kuwa Rais?
4. Kitendo cha mwajiriwa wa upande wa mdhamini kuwania urais hakiwezi kusababisha wanachama kutopiga kura kwa uhuru kwa hofu ya kutomkasirisha mdhamini?
5. Ikiwa Injinia atashinda, ataweza kumwajibisha mdhamini ambaye ni kampuni anayofanyia kazi ikiwa atakiuka baadhi ya vipengele vya kimkataba baina yake na klabu?