Wakati uongozi wa Simba ukiwa katika harakati za mwisho ili kuweka wazi jina la kocha Mkuu anayechukua nafasi ya Pablo Franco, makocha wameshauri kocha aliyesalia Seleman Matola kumpa mwongozo mgeni huyo atakapotua nchini.
Matola amekuwa na bahati ya kusalia ndani ya benchi la ufundi hasa pale makocha wenzake wakuu wanapofungashiwa virago akiwa chini ya Patrick Ausseums, Didier Gomes, Pablo Franco pamoja na Sven Vandenbroeck.
Jamhuri Kihwelu Julio ambaye Kocha wa zamani wa Simba alisema; “Kocha anayekuja akiambiwa na Matola kuna hawa wanahitajika atamsikiliza zaidi,”
“Tatizo kubwa lililopo kwa timu hizi kubwa Simba na Yanga sio makocha wanaosajili, wachezaji wengi wanasajiliwa na viongozi kwa mihemko na matakwa yao binafsi na ndio maana ukimshauri hivi kunakuwepo na dharau nyingi kwa kujua kaletwa na mtu fulani,”alisema.
Kocha Kessy Mziray aliyekuwa akiinoa Alliance FC alisema; “Madhara makubwa ya kukuta wachezaji ambao sio chaguo lako ni ngumu kuendana na falsafa yako, kwani wachezaji ndio wanatengeneza mfumo na si mfumo kutengeneza wachezaji, hizo timu kubwa viongozi ndio wanasajili na sio kocha hivyo sioni ugumu wa kocha ajaye Simba.” Kocha wa Geita Gold Fredy Felix ‘Minziro’ alisema, “Ni changamoto kutosajili mwenyewe.”