Home Habari za michezo BAADA YA KUTOONEKANA GEITA FC…SINGIDA BIG STARS WAMKANA NCHIMBI MCHANA KWEUPEEE…”HATUNA MPANGO...

BAADA YA KUTOONEKANA GEITA FC…SINGIDA BIG STARS WAMKANA NCHIMBI MCHANA KWEUPEEE…”HATUNA MPANGO NAYE”….


Uongozi wa Klabu ya DTB FC (Singida Big Stars) umekanusha taarifa za kuwa kwenye mchakato wa kumsajili Mshambuliaji wa Geita Gold FC Ditram Nchimbi.

Singida Big Stars itakayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao (2022/23), imekua ikitajwa kujipanga kufanya usajili mkubwa ili kutoa upinzani kwa timu za Ligi Kuu na ikiwezekana kumalizia katika nafasi za juu.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Klabu hiyo itakayotumia Uwanja wa Liti (Namfua-Singida) kama Uwanja wake wa nyumbani, Muhibu Kanu amesema taarifa za usajili wa Nchimbi sio za kweli, na hakuna mpango wowote wa kumsajili Mshambuliaji huyo.

Amesema Singida Big Stars ina mipango yake ya usajili, na muda utakapowasia kila kitu kitawekwa hadharani, na wadau wa soka watafahamishwa kupitia vyanzo mbalimbali vya habari vya klabu hiyo.

“Suala la Kumsajili Nchimbi sio la kweli, kuna uzushi unaendelea kwenye mitandao ya kijamii na sisi kama viongozi tunauona, mashabiki wa klabu yetu wanapaswa kuwa watulivu kwa sababu tuna mipango mizuri ya usajili,”

“Tutakaowasajili watafahamika kupitia vyanzo vyetu vya habari, wachezaji watasajiliwa hilo ni lazima, lakini sio kwa mpango huu wa taarifa kuzushwa kwenye mitandao ya kijamii.” amesema Muhibu Kanu.

Nchimbi kwa sasa hayupo kwenye kikosi cha Geita Gold FC iliyomsajili Mwezi Januari 2022, kwa madai ya kutomaliziwa sehemu ya fedha yake ya usajili.

DTB FC (Singida Big Stars) ilimaliza nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiungana na Ihefu FC iliyomaliza kinara kwenye msimamo wa Ligi Daraja la Kwanza msimu huu 2021/22, kupanda Ligi Kuu msimu ujao 2022/23.

SOMA NA HII  FEISAL SALUM ""FEI TOTO" ATENGWA NA KIKOSI...ANAPEWA MAZOEZI PEKE YAKE