Home Habar za Usajili Simba PAMOJA NA KUMALIZANA NA MOSES PHIRI…TRY AGAIN AIHOFIA AL AHLY YA MISRI...

PAMOJA NA KUMALIZANA NA MOSES PHIRI…TRY AGAIN AIHOFIA AL AHLY YA MISRI KUWAIBIA MASTAA WANAOWATAKA…


Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba wameendelea kukisuka kikosi chao kimyakimya kuelekea msimu ujao wa 2022/ 23, na tayari wamemaliza kazi kwa mshambuliaji wa Zanaco ya Zambia, Moses Phiri, imefahamika.

Licha ya Klabu ya Simba kuendeleza utamaduni wake wa kutaka kuwatangaza wachezaji wanaowasajili kwa utaratibu maalum pindi dirisha la usajili litakapofunguliwa, lakini  taarifa za uhakika kuhusu mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, kumalizana na Phiri.

Phiri ambaye anatisha kupachika mabao, amejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Zanaco na rasmi ataanza kuvaa jezi nyekundu na nyeupe Simba msimu ujao.

Chanzo chetu cha uhakika ndani ya klabu hiyo kimemweleza mwandishi wetu kuwa mshambuliaji huyo amemalizana na Simba licha ya wapinzani wao, Yanga nao awali kutaka kuingilia dili hilo.

“Simba ilishakubaliana na Phiri tangu usajili wa dirisha dogo, lakini dili hilo lilishindikana kutokana na klabu yake kukabiliwa pia na michuano ya kimataifa, hivyo haikuwa tayari kumwachia kwa wakati huo,” kilieleza chanzo chetu huku kikiomba hifadhi ya jina lake.

“Hata hivyo, wapinzani wao…nao walitaka kumsajili lakini waligonga mwamba baada ya kutajiwa dau kubwa, lakini mchezaji mwenyewe alionyesha kuwa na mapenzi zaidi na Simba.”

Lakini pia katika Wikipedia ya Phiri, nayo inaonyesha klabu yake ya sasa ni Simba Sports Club. Phiri mwenye umri wa miaka 29, sasa ataungana na nyota wenzake wawili kutoka Zambia ndani ya kikosi cha Simba, viungo Rally Bwalya na Clatous Chama ambao wote wanaichezea timu yao ya taifa.

Katika kile kinachoonekana hawataki mipango yao kuingiliwa, mwishoni mwa wiki Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Klabu ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’, baada ya tetesi nyingi za usajili kuvuma huku wakidaiwa kuzidiwa ujanja na watani wao, Yanga katika mbio za kumsajili kiungo mshambuliaji wa Asec Mimosas ya Ivory Coast, Stephane Aziz Ki, alisema kwa sasa mambo yao ya usajili wanayapeleka kimyakimya.

“Tumejifunza kuwa na weledi mkubwa kwenye usajili, maana wapinzani wetu, Al Ahly, Orlando, Berkane wanafuatilia kila tunapopiga hodi. Sasa kama tutakuwa tunatembea na kamera kupiga picha na wachezaji tunaowafuatilia, itakuwa shida, wanachama na mashabiki wa Simba tuachieni sisi kazi ya kusajili,” alisema.

SOMA NA HII  DILI LA IDUMBA KUTUA SIMBA LIMEFIKIA HATUA HII...UNAAMBIWA NI BEKI HASWA...MAYELE HAPITI...

Rais wa Heshima na Mwekezaji wa klabu hiyo, Dk. Mohammed “Mo” Dewji, tayari ametangaza kutenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya usajili ili kukiimarisha kikosi cha timu hiyo kuelekea msimu ujao wa michuano iliyopo mbele yao hususan Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mbali na usajili wa wachezaji, Simba pia ipo katika harakati za kusaka kocha mpya baada ya kumtimua kazi Kocha Mkuu, Mhispania Pablo Franco kwa kile kilichoelezwa ni kushindwa kufikia malengo aliyowekewa ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu, Kombe la FA na kufika nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.