Home Habari za michezo KUELEKEA MSIMU UJAO…TARAJIA KUKIONA KIFAA HIKI CHA KAZI KIKIPIGA KAZI MSIMBAZI…ISHU NZIMA...

KUELEKEA MSIMU UJAO…TARAJIA KUKIONA KIFAA HIKI CHA KAZI KIKIPIGA KAZI MSIMBAZI…ISHU NZIMA IKO HIVI…


Simba haijapoa. Mabosi wao wanazidi kukuna kichwa ili kutengeneza timu itakayofukia mashimo yote yaliyojitokeza msimu huu na kushindwa kutimiza malengo yao na moja ni kusaka wachezaji wa kiwango cha juu wa kuweza kurejesha heshima hiyo.

Kama wewe ni shabiki wa Simba, basi zikufikie tu taarifa, mabosi wa klabu hiyo mezani kwao wana majina wanne ya viungo washambuliaji ambao mmoja wao atashushwa mambo yakikamilika ambaye ni Morlaye Sylla anayekipiga kwa sasa AC Horoya ya Guinea.

Sylla aliyewahi kucheza soka la kulipwa Ureno, ni moja kati ya machaguo matatu ya kwanza katika majina hayo manne na Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez amewatuliza mashabiki wa timu hiyo akiwaambia kuna mambo mazuri yapo njiani.

Chanzo makini kutoka ndani ya Simba, kimedokeza kuwa raia huyo wa Guinea anapigiwa hesabu na mabosi wa Simba kutokana na kumfuatilia kwa muda mrefu ili kumshusha Msimbazi, akiwa ni chaguo la tatu.

Kiwango anachoonyesha Sylla kwenye timu ya taifa pamoja na klabu yake ya Horoya kinatajwa ndicho kilichowavutia mabosi wa Simba na kuanza mchakato wa kumfuatilia kwa kutafuta taarifa zake mbalimbali.

“Kweli tunahitaji kiungo mwingine mshambuliji aliyekuwa kwenye kiwango bora kwa sasa na Sylla ametuvutia, ngoja tuone kama inawezekana kupatikana kwani ni mmoja wa wachezaji wazuri,” kilisema chanzo chetu makini (jina limehifadhiwa).

“Tunahitaji kiungo aina ya Sylla ili kuongeza nguvu mbele ya Clatous Chama na Rally Bwalya ambaye huenda tusiwe naye msimu ujao kutokana na dili lake la kuuzwa Amazulu limefikia mahala pazuri.”

Sylla amekuwa kwenye kiwango bora kwenye Ligi Kuu ya Guinea ikionyesha ubunifu wa kupiga pasi za mwisho, kuanzisha mashambulizi, mzuri anapokuwa na mpira mguuni, mbunifu pamoja na kuwasumbua viungo wa timu pinzani.

Kiungo huyo alianza soka la vijana katika klabu ya E. Tanene kisha kutua Arouca ya Ureno kabla ya kurudia CO de Coyah ya kwao Guinea mwaka 2019 kabla ya kutua AC Horoya aliyonayo hadi sasa.

SOMA NA HII  BAADA YA KICHAPO CHA ZANACO...YANGA WAJIPOOZA LEO..WAICHAPA TIMU YA DARAJA LA KWANZA GOLI ZA KUTOSHA

Akiwa na umri wa miaka 23 tu, tayari mwamba huyo ameshachukua tuzo mbalimbali ikiwemo za mchezaji bora wa mechi, huku akizichezea timu za taifa ya Guinea akianza na timu ya vijana U17 mwaka 2015 na kucheza mechi tatu na kufunga nao moja.

Pia amewahi kukipiga U20 2017 akicheza mechi nane na kufunga mabao mawili na sasa yupo timu ya wakubwa akiichezea michezo nane na kufunga mabao matatu.

Simba inahitaji kiungo wa ushambuliaji raia wa kigeni kutokana na kutofurahishwa na wachezaji wanaocheza kwa sasa katika eneo hilo msimu huu wakiwemo, Chama, Bwalya na wengineo.

Machaguo mawili ya kwanza kwa mabosi wa Simba walipanga kumsajili, Victorien Adebayor wa USGN na Stephane Aziz Ki na imekuwa ngumu kwao kutokana na nyota hao kuhitajika na timu nyingine ikiwamo Yanga na RS Berkane.

Adebayor anaweza akatua RS Berkane ya Morocco iliyomwekea mkwanja mrefu zaidi ya ule ambao Simba inaweza kutoa, wakati Ki wa Asec Mimosas inaelezwa huenda akatua Yanga.

MSIKIE BARBARA

Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alipotafutwa kuzungumzia juu ya usajili wa nyota wapya, alisema suala la usajili wanalishughulikia kwa umakini mkubwa na kwa sasa wapo kwenye vikao na timu yake ili kuona namna gani wanaweza kupata wachezaji wazuri.

“Tunaendelea na mchakato, tunatafuta wachezaji wazuri na muda si mrefu mambo yatakuwa sawa na tutawaeleza kuhusu hili kupitia mitandao ya kijamii ya Simba. Mtajua kama watakuja wachezaji gani, ila wapo tunaozungumza nao ambao siwezi kuwataja kwa sasa,” alisema.

Simba ilishalitema taji lao la ASFC walilokuwa wakilishikilia kwa misimu miwili mfululizo, huku ubingwa wa Ligi Kuu iliyoishikilia kwa misimu minne mfululizo unaelekea kuwaponyoka kutokana na Yanga kuwa na nafasi kubwa ya kulitwaa ikiwa kileleni mwa msimamo na pointi 64.