Home Habari za michezo RAIS SAMIA ABARIKI TANZANIA KUOMBA KUANDAA AFCON 2027…AHAIDI UJENZI WA VIWANJA...

RAIS SAMIA ABARIKI TANZANIA KUOMBA KUANDAA AFCON 2027…AHAIDI UJENZI WA VIWANJA VIPYA VITATU…


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema atakuwa mstari wa mbele kuhakikisha Tanzania inatimiza vigezo vya kupata viwanja sita vitakavyokidhi kupewa uwenyeji wa Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2027.

Kauli hiyo aliitoa Ikulu jijini Dar es Salaam jana wakati wa hafla ya kupokea Kombe la Dunia, ambayo alikuwa mgeni rasmi wa shughuli hiyo itakayoendelea leo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa Watanzania wote watakaojitokeza kupata fursa ya kupiga nalo picha.

Rais Samia alisema ili kupata nafasi ya kuandaa michuano ya Afcon 2027, lazima Tanzania iwe na viwanja sita huku tayari ikiwa na vitatu ambavyo alivitaja kuwa ni Benjamini Mkapa, Uhuru vilivyopo Dar es salaam na Uwanja wa Amaan ulioko visiwani Zanzibar.

“Ili tufanye mashindano hayo ya AFCON lazima tuwe na viwanja sita vyenye sifa hadi sasa tunavyo vitatu, tunatakiwa kupata vitatu vingine, kwa hali hiyo nitakuwa bega kwa bega na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kuhakikisha tunapata viwanja vingine,” alisema na kuongeza;

“Hadi sasa tayari tumeshakuwa na uhakika wa kupata uwanja mmoja baada ya kampuni mbili ikiwamo Coca Cola na nyingine kusaidia mchakato wa kupata uwanja wa nne, lakini tunatakiwa kupata hoteli na miundombinu ili tuwe wenyeji wa mashindano ya AFCON 2027.”

Rais alisema anaipongeza Wizara ya Michezo kwa kupambana na kuhakikisha inapata nafasi ya kuwa mwenyeji wa mkutano wa CAF, utakaofanyika Agosti mwaka huu na kuitaka waitumie fursa hiyo kutangaza nchi na biashara kwa kuwalisha wageni vyakula vya Kitanzania.

“Ningependa kuwapo katika mkutano huo utakaokutanisha viongozi wa soka wa CAF, FIFA na viongozi wa nyama vya soka, tuombe kati ya hizo tarehe nisiwe na majukumu mengine,” alisema Rais Samia.

Alisema ujio wa Kombe la Dunia nchini unapaswa kuwa chachu kwa wachezaji na wadau wa soka kufanya vizuri zaidi katika mchezo wa mpira wa miguu.

“Hii ni siku ya kipekee kwa kupokea Kombe la Dunia, nimefurahi kumuona Juliano Belleti, amewahi kutwaa Kombe la Dunia (akiwa na Brazil), nimefurahi kuona kabla ya kwenda Qatar kombe limepita hapa.

SOMA NA HII  ILE ISHU YA PABLO KUTAKIWA NA ORLANDO...WAKALA WAKE MKENYA AIBUKA NA KUANIKA KILA KITU WAZI...

“Timu za wanawake na vijana zimekuwa zikifanya vema katika michezo, lakini umaliziaji umekuwa duni kombe hili linapaswa kututia moyo na kuwatayarisha vijana wetu kufanya vyema,” alisema.

“Kama nchi tumefurahi kupokea kombe hilo na ninawaomba vijana wajitokeze kwa wingi ili waweze kutazama na kupiga picha,” alisema Rais Samia.

Naye Mkurugenzi wa Coca Cola Kwanza, Unguu Suley, alisema kuwa Coca Cola, wanatoa shukrani zao kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kukubali kuwa mwenyeji na kulipokea Kombe la Dunia.

“Hii ni historia muhimu kwetu ikiwa ni miaka nane imepita baada ya Kombe la Dunia kuja hapa nchini huku ukiwa rais wa kwanza mwanamke kulipokea kombe hili, kwani katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wako kuna mafanikio mengi kwenye mchezo wa soka,” alisema Suley.